
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dkt. Abiy Ahmed Ali amewasili nchini leo Februari 29, 2024 kwa ajili ya ziara yake ya kitaifa ya siku tatu.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Abiy amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.
Dkt. Abiy atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam kesho, Machi Mosi, 2024.

Pamoja na mambo mengine, ziara ya Waziri Mkuu Abiy inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Ethiopia katika maeneo ya kimkakati ikiwemo usafirishaji kwa njia ya anga, nishati, kilimo na mifugo, biashara na uwekezaji na Ushirikiano katika sekta za elimu, uhamiaji, na ulinzi na usalama
Ziara hiyo ambayo itakamilika Machi 2, 2024 inafanyika kufuatia mwaliko wa Rais Samia.
