×

Chama Cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania TWCC Chahimiza Wanawake Kushiriki Tuzo Za Viwanda

Mkurugenzi wa TWCC Bi. Mwajuma Hamza (kulia) akizungumza kwenye mkutano huo. Katikati ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la TradeMarkAfrica Ndugu. Elibariki Shammy na kushoto ni Mwenyekiti wa TWCC Bi.Mercy Sila.

Dar es Salaam, 5 Machi, 2024: Chama cha Wanawake WafanyabiasharaTanzania (Tanzania Women Chamber of Commerce -(TWCC) leo kimefanya mkutano na vyombo vya habari na kuhimiza ushiriki wa wanawake wajasiriamali na wafanyabiashara katika kuwania tuzo za Viwanda na Biashara msimu wa nne ambazo zinaambatana na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani 2024. Tuzo hizi zitatolewa tarehe 16 Machi, 2024 katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki -Dar es salaam.

Malengo ya tuzo hizo ni pamoja na;

  • Kutambua wanawake waliofanikiwa na wale wanaochipukia katika sekta za viwanda na biashara.
  • Kujenga imani juu yaujasiriamali na kuhamasisha wanawake wa vizazi vijavyo kuwekeza na kujishughulisha katika shughuli za viwanda na biashara.
  • Kusheherekea mafanikio wanayoyapata wanawake katika sekta za viwanda na biashara.

Katika kuhimiza wanawake kushiriki Tuzo hizi ambazo zinaandaliwa kwa mara ya nne mfululizo, Mkurugenzi wa TWCC Bi. Mwajuma Hamza  amesema‘’Tuzo hizi zinalenga kuonesha mchango wa mwanamke mjasiriamali katika kukuza uchumi wa nchi na kuchochea maendeleo ya jamii’’. Aliongeza kuwa ‘’wanawake ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya jamii yoyote na kwamba wanawake wanauwezo wakufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda na biashara endapo wataendelea kuaminiwa na kupewa nafasi yakufanya hivyo’’. 

Mchakato wa upatikanaji wa washindi wa tuzo umeanza tangu tarehe 20 Februari, 2024. Hivyo TWCC inahimiza wanawake wajasiriamali kuendelea kujisajili kwa kujaza fomu ambayo inapatikana bure katika tovuti ya TWCC www.twcc-tz.org, pamoja na ofisi za TWCC katika Mikoa yote. Aidha, mwaka huu TWCC imetoa nafasi kwa wananchi kupendekeza wanawake vinara kwenye biashara na hasa wale wanaokidhi vigezo vilivyowekwa ili waweze kuingizwa kwenye mchakato wa kushindania Tuzo hizi.

Mkurugenzi wa TWCC Bi. Mwajuma Hamza akisisitiza jambo.

Jumla ya vipengele au kategori 20 zinashindaniwa kutoka kwenye sekta mbalimbali kama vile; Kilimo,Uzalishaji, Madini, Usafirishaji, Biashara ya kuuza nje ya nchi, Biashara za kuvuka Mipaka, Huduma za kifedha, Ujenzi, Afya, Elimu, Utalii, Uhandisi, Mawasiliano, Sanaa, Teknolojia ya habari, Uvuvi,Usimamizi wa hafla, Huduma za Chakula (Mama Lishe), Ufugaji na Branding.

Mwisho wa kujaza fomu za kuwania tuzo ni siku ya ijumaa tarehe 8 Machi, 2024.

Aidha, Mwenyekiti wa TWCC Bi.Mercy Sila ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ambapo wanawake wengi wameweza kuanzisha biashara na viwanda vidogo ambavyo vimewaongezea kipato, kuzalisha ajira pamoja kuchangia katika kukua kwa uchumi wa nchi.

‘’Kipekee kabisa nimshukuru Mhe. Rais wetu Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kufungua nchi na kuboresha mazingira ya uwekezaji Nchini. Sisi wanawake tumeendelea kutumia fursa kikamilifu na kupitia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kila mwaka ndipo tunapata nafasi ya kutathmini mafanikio ya wanawake, vikwazo Pamoja na kuweka mikakati ya kuendeleza biashara zao’’ amesema Bi.Mercy Sila.

‘’Naomba nitoe shukurani kwa wadau wetu wote ambao wameendelea kujitokeza kudhamini Tuzo hizi Pamoja na matukio yote ambayo TWCC imekua ikiandaa katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani kila mwaka. Kipekee Nipende kuwashukuru TradeMark Afrika (TMA) kwa kuendelea kudhamini shughuli za wanawake pamoja na Tuzo hizi’’-Bi.Mercy Sila.

Mdhamini Mkuu wa Tuzo za mwaka huu kwa mara ya nne ni TradeMark Africa (TMA) chini ya mradi wa kujengea wanawake uwezo wakufanya biashara. TMA wamekuwa wakifadhili TWCC toka mwaka 2012 ili kujenga uwezo wanawake kuuza bidhaa ndani ya Jumuiya ya Afrika mashariki. Kupitia udhamini huu wanawake wengi wameweza kufikiwa na kujengewa uwezo.

Nae Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la TradeMarkAfrica Ndugu. Elibariki Shammy amesema, kwakipindi cha mwaka 2016 mpaka 2023, TMA iliwekeza Zaidi ya Shillingi Billion 7.5 kujengea wanawake wa Tanzania uwezo wakufanya biashara na hasa biashara za mipakani. Kwakipindi hicho zaidi ya wanawake 20,000 walifikiwa na mradi huo kupitia TWCC.

Kwakipindi cha mwaka 2024 mpaka 2030 , TMA imetenga zaidi ya Shillingi Billion 4 ambazo zitatumika kuendelea kujengea wanawake uwezo wakufanya biashara. 

‘’TMA imekuwa ikifadhili tuzo hizi za wanawake kwa miaka minne sasa. Tuzo hizi zimekuwa chachu ya wanawake wengi zaidi kuingia kwenye biashara nakuongeza vipato vyao. Wakati mwingine mazingira ya biashara yanaweza kuwa magumu hasa kwa wanawake.

Vilevile, mazingira katika familia zetu wakati mwingine hayatoi nafasi yakutosha sana kwa wanawake kutumia muda wao mwingi kwenye biashara. Tuzo hizi ni jukwaa lakutoa ujumbe kwa wanawake wengi zaidi kuwa inawezekana wanawake zaidi kuingia kwenye biashara na kufanikiwa’’.

‘’TMA itaendelea kushirikiana na TWCC kuendeleza ukuaji wa tuzo hizi nakuona kuwa zinaendelea kuwa nguzo ya uhamasishaji wanawake kuingia kwenye biashara za kitaifa, kikanda na kimataifa.”,aliongeza Mkurugenzi Mkazi -TMA

HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL

Leave a Comment