×

Marekani na Tanzania Zaandaa Kwa Pamoja Kongamano la Intelijensia ya Kijeshi

Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani (AFRICOM) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliandaa kwa pamoja na kuwa wenyeji wa Kongamano la Wakuu na Wakurugenzi wa Intelinsia za Kijeshi (Chiefs & Directors of Military Intelligence Conference -CDMIC) uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania, kuanzia Aprili 30 hadi Mei 3.

Wazungumzaji wakuu wakuwa ni pamoja na Brigedia Jenerali wa Jeshi la Marekani Rose Keravuori, Mkurugenzi wa Intelijensia wa AFRICOM, pamoja na Mkuu wa  Intelijensia wa JWTZ, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy.

Kongamano la mwaka 2024 liliangazia dhamira ya dhati ya AFRICOM katika kujenga ushirikiano na washirika wa Afrika, ukisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kiintelijensia na maslahi ya pamoja. Likiwa jukwaa muhimu, kongamano hili liliwezesha kuweka mikakati ya pamoja kukabiliana na changamoto mbalimbali barani Afrika.

Zaidi ya hayo, kongamano lilisaidia kuimaarisha mfumo wa utendaji jumuishi wa AFRICOM unaohusisha serikali yote (whole-of-government approach) kwa kujumuisha diplomasia, maendeleo, na ulinzi katika ushirikiano wake na wabia wake wa Kiafrika.

Brigedia Jenerali Keravuori alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa kupeana/kubadilishana  taarifa kwa wakati, akitambulisha dhana mpya ya kibunifu ya diplomasia ya kiintelijensia.

Alisema mbinu hii inatumia taarifa za kiintelijensia kama zana muhimu ya kusaidia katika kufanya maamuzi, kuwezesha ushirikiano wa kimkakati na kuwa na mitazano ya pamoja, kuwezesha kuchukua hatua za pamoja, na kuwanyima maadui fursa ya kufaidika isivyostahili.

“Simu zenu zitapokelewa kwa furaha, na mitazamo yenu itazingatiwa kwa makini,” alisema Keravuori, akisisitiza dhamira ya kamandi ya kuwa na mawasiliano ya wazi.

Katika kongamano hili, washiriki kutoka mataifa 33 ya Kiafrika walikusanyika kujadili mada muhimu mbalimbali kama vile: Changamoto za vitisho mbalimbali vya kiusalama barani Afrika; ugaidi na uhalifu mkubwa wa kupangwa (Organized crime) barani Afrika: kuendesha shughuli pamoja na ushirikiano; intelijensia ya kijeshi katika maeneo ya bahari: na kuwezesha kutoa onyo la mapema (early warning) dhidi ya vitisho mbalimbali.

Jenerali João Pereira Massano, mkuu wa Huduma za Kiintelijensia na Usalama wa Jeshi la Angola na mwenyeji mwenza wa CDMIC ya 2023, alikubaliana na maoni hayo.

“Upatikanaji wa taarifa kupitia mitandao mipana ya uhusiano hujenga na kuwezesha mabadilishano muhimu ya taarifa na maarifa,” alisema.

Katika hotuba yake, Meja Jenerali Mkeremy alizungumzia umuhimu wa ushirikiano, akiutaja ushirikiano huo kuwa na jukumu la pande mbili, jukumu la kuwa marafiki kwa upande mmoja na wakati huo huo kuwa ndugu.

“Lengo letu la pamoja ni kushirikiana kutengeneza suluhisho linalotokana na kuongozwa na Waafrika wenyewe kwa changamoto zilizopo, huku tukilenga kupanua fursa kwa vijana wetu na kuleta ustawi kwa wote,” alisema Meja Jenerali Mkeremy.

Mvemba Phezo Dizolele, mtafiti mwandamizi na mkurugenzi wa Programu ya Afrika katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa, alisisitiza umuhimu wa diplomasia ya kiintelijensia katika kukabili na kushughulikia wigo unaoongezeka wa vitisho vya kimataifa, kuanzia uhalifu wa kimkakati hadi ugaidi na changamoto za kidijitali.

Dizolele alisema diplomasia ya kiintelijensia ni zana muhimu kwa nchi kuunda ushirikiano wa manufaa ya pamoja dhidi ya changamoto hizo. Makongamano kama CDMIC yana nafasi muhimu katika kukuza ushirikiano wenye ufanisi wa kiintelijensia unaojengwa katika misingi ya kuaminiana. Hatimaye, alihitimisha Dizolele, ushirikiano wa kiusalama unajengwa katika misingi ya kuaminiana.

Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani, yenye makao yake makuu Stuttgart, Ujerumani, ni mojawapo ya kamandi 11 za Wizara ya Ulinzi ya Marekani. Kila moja ikiwa na majukumu ya kijiografia au kitendaji ya kuamrisha na kudhibiti vikosi vya kijeshi wakati wa amani na vita. AFRICOM inatumia mbinu ya diplomasia, maendeleo, na ulinzi ili kuimarisha juhudi za taasisi na kusaidia kudhibiti vyanzo na vichocheo vya migogoro na ugaidi barani Afrika.

 

Source: US EMBASSY IN TANZANIA

Leave a Comment