
Dar es Salaam 7 Mei 2024: Tamasha kubwa la kimataifa la utamaduni na utalii linalojulikana kama Lake Zone Cultural and Tourism Festival limezinduliwa rasmi Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwafikia washiriki wengi zaidi.
Uzinduzi huu unakuja ukiwa umebaki mwezi mmoja tu kabla ya tamasha hilo la aina yake kufanyika huko Bariadi Mkoani Simiyu.
Uzinduzi huo umefanywa na kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours ambao ndio waandaaji wakuu na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo Baraza la Sanaa Tanzania, Bodi ya Utalii Tanzania, wadau wa utamaduni kutoka Bariadi, Simiyu na waandishi wa habari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro One Travel and Tours, Christina Emmanuel amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo ambayo inajihusisha na masuala ya utalii na utamaduni kuandaa tamasha hili ambalo litakuwa na muitikio mkubwa kwa wakazi wa Simiyu na mikoa ya jirani.

“Tamasha hili linatarajiwa kufanyika mwezi wa saba na ninayo furaha kukufahamisha kuwa litafanyika kwa siku tatu mfululizo Julai 5, 6 na kilele chake kitakua Julai 7 ambapo pamoja na mambo mengine tunategemea kuwa na maonyesho mbalimbali ya masuala ya utamaduni na utalii katika Uwanja wa Halmashauri na kuwavutia washiriki na watazamaji zaidi ya 7,000 kwa siku hizi tatu,” alisema.

Aliongeza litakuwa na vionjo mbalimbali ikiwemo ngoma inayohusisha makabila ya Wagika na Wagulu, maonyesho, michezo mbalimbali na vyakula” ameongeza.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. Mohamed Hatibu naye alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara, makampuni, taasisi na mashirika kujitokeza na kuunga mkono kama njia moja wapo pia ya kuiunga mkono Serikali katika kuutangaza utamaduni na utalii wa Simiyu.
“Tumejiandaa vizuri na tuna uhakika tamasha hili litafanikiwa na litakuwa na kila mwaka,” alisema na kusema kuwa tamasha hilo linatarajiwa kuwavutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa wa BASATA, Bw. Edward Buganga amewasifu waandaaji kwa kuandaa tamasha hilo katika kuendeleza utamaduni na Utalii hapa nchini, akitoa wito kwa wadau wengine kuliunga mkono tamasha hilo kwa hali na mali.
“Ni tamasha kubwa la aina yake ambalo sisi kama Watanzania tunapaswa kujivunia kuwa hili ni tamasha la kwetu kwa maendeleo ya utamaduni na utalii wetu,”alisema na kusisitiza kuwa Basata itatoa ushirikiano mkubwa kwa waandaaji ili tamasha hilo lifanyike kwa ufanisi mkubwa.
Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Bw.Nassor Garamatatu aliipongeza Kilimanjaro One Travel and Tours kwa kuona umuhimu wa kuunganisha utalii na utamaduni kwani haviwezi kutenganishwa.
“Sasa hivi sisi kama bodi tumejikita sana katika kutangaza utalii wa utamaduni ndio maana tuko tayari kuliunga tamasha hili mkono ili tutangaze utamadunina vivutio vya utalii kwa mkoa wa Simiyu.
Baadhi ya wabia na wadhamini wa tamasha hili ni pamojja na Tigo, NMB Bank, Z & M General Traders, Widescope Interprises Limited, na Carehealth and Hospitality Services.