
Nabii Domonic maarufu Kiboko ya Wachawi anayeendeshea huduma za kinabii na uponyaji kwenye kanisa lake lililopo Buza jijini Dar wikiendi iliyopita aliwafanyia Surprise wanahabari kwa kufanya nao mkutano katikati ya bahari kwa kutumia boti ya kisasa ‘Yatch’ iliyokuwa ikitembea kuanzia ufukwe wa Msasani eneo la Slipway.
Katika mkutano huo uliokuwa na lengo la kuutangaza mkesha mkubwa wa kuliombea taifa pamoja viongozi wake wanaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ulikuwa ukiendelea huku wanahabari na msafara Kiboko ukiinjoi mandhari ya fukwe za jiji.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Kiboko ya Wachawi alisema lengo kufanyia mkutano huo kwenye boti hiyo ya kifahari ni kuwapa hadhi yao wanahabari ambao wengine huwachukulia kirahisi lakini yeye anawapa thamani ya juu sana na anafikiria siku nyingine kufanya nao mkutano kwenye chombo cha angani.

“Wanahabari ni watu muhimu sana katika jamii na mimi binafsi natambua sana mchango wao katika jamii ndiyo maana nimeonelea leo tuanzie na kufanya mkutano hapa baharini na siku nyingine nitaangalia sehemu nyingine hata angani kwa kutulia flight”. Alisema Kiboko ya Wachawi.
Baadhi ya wanahabari waliozungumza na Global baada ya mkutano huo walisema wameiona siku hiyo kama ni siku ya bahati kwao kwa kuvinjari kwenye boti hiyo inayotumiwa zaidi na watu wanaoishi maisha ya fahari.