
ALAF Limited, kampuni inayoongoza na inayoaminiwa kwa kuzalisha vifaa vya ujenzi Tanzania, Jumamosi ilizindua Maonyesho ya kazi kwenye Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DTI).
Meneja wa Rasilimali watu wa ALAF Bw. Jumbe Onjero alisema uzinduzi huo wenye dhamira ya ‘Kujenga Madaraja’ ulilenga kukuza vipaji vya vijana ili kupata mafanikio katika maisha yao.
Bw Onjero alisema: “Dhamira ya ‘Kujenga Madaraja’ inaonyesha moyo wetu wa dhati wa kuanzisha mahusiano imara na ya kudumu na wanafunzi wetu, wanaojiandaa kwa kazi na kwa mahitaji ya tasnia,” alisema.
Kulingana na Bw. Onjero alisema maonyesho ya taaluma ni fursa nzuri kwa watu binafsi kusikia masimulizi ya mafanikio ya ukuaji wa kazi, kuwa na mtandao wa mawasiliano na wanataaluma hao na kujifunza zaidi kuhusu ujuzi unaohitajika ili watu waweze kufikia malengo ya kazi zao.

Alisema baada ya DIT, ALAF inaarajia kwenda katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu, kama vile vyuo vikuu na vyuo vingine na shule za sekondari nchi nzima.
“Tukio la Jumamosi lilikuwa na hotuba kutoka nyanja mbalimbali, warsha shirikishi, na mijadala ya paneli, kipindi cha ‘maswali na majibu’ kilichoratibiwa vyema, kikiruhusu kushirikishana uzoefu binafsi wa washiriki.”
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Taaluma wa DIT aliipongeza ALAF Limited kwa kuanzisha maonyesho ya taaluma, akisema ni njia nzuri ya kurudisha kwa jamii ukarimu.
“Hii itahakikisha wanafunzi wetu wanajiandaa vizuri kukabiliana na soko la ajira na wanajua matarajio ya jamii kwao watakaofika huko kwenye soko,” alisema.

Alisema kitendo cha kuwaleta wanafunzi waliopita DIT na sasa wameajiriwa na ALAF kimewatia moyo wanafunzi wanaotarajia kumaliza masomo Yao.
Mmoja wa wanafunzi hao wa zamani, Injinia Tumaini Minja, alisema Programu hii ya ALAF ilimfungulia fursa kwani aliajiriwa mwaka mmoja baada ya kufanya kama majaribio na baada ya miaka Saba sasa anasimamia kitengo cha mabati ya rangi.

“ALAF imeona umuhimu wa kuajiri vijana wa kitanzania Kwa maana hiyo wameweka nguvu kubwa katika career fair ili wapate watu sahihi,” alisema.
Waziri wa Miundombinu na Teknolojia wa DIT, Kelvin Wilson ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne anayesomea uhandisi wa umeme, alisema zoezi hili ni la kuigwa kwani litahakikisha ALAF inapata mainjinia wa uhakika.