Benki ya CRDB imeungana na wadau wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wajasiriamali Duniani (International MSMEs Day) kwa kuendesha semina kwa wateja wake na baadhi ya wabia wa kimkakati.

Sherehe za maadhimisho hayo zimefanyika makao makuu ya Benki hiyo yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya wajasiriamali 300 wameshiriki.
Akifungua maadhimisho hayo Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile amesema Benki hiyo imeweka mkazo mkubwa katika uwezeshaji wa wajasiriamali nchini kupitia huduma na bidhaa bunifu zikijumuisha utunzaji wa amana, mifumo ya malipo, na mafunzo.

Mwile amesema hadi mwishoni mwa Mei 2024, Benki hiyo imetoa mikopo yenye jumla ya thamani ya Sh. bilioni 995.346 kwa zaidi ya wajasiriamali 21,470 katika sekta mbalimbali uchumi.
Mwile amewakaribisha wajasiriamali kote nchini kuchangamkia fursa zinazotolewa na Benki hiyo na kusema kuwa imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya uwezeshaji wa kundi hilo la wateja.
Kwenye sherehe hizo pia Benki ya CRDB imezindua akaunti maalumu kwa ajili ya wajasiriamali wadogo ijulikanayo kama CRDB Biashara Account kuwasaidia kutunza akiba, kupitisha miamala ya mauzo pamoja na malengo mengine ya kukua kiuchumi.

Taarifa za Umoja wa Mataifa (UN) zinasema sekta ya ujasiriamali inachangia asilimia 90 ya biashara zote zilizopo duniani ambazo hutoa kati ya asilimia 60 mpaka 70 ya ajira zenye staha na kuchangia zaidi ya nusu ya pato la dunia. Tanzania kuna zaidi ya wajasiriamairi milion 3.2, ambapo sekta hiyo inachangia asilimia 27 ya Pato la Taifa (GDP).