
Dar es Salaam 2 Julai 2024: Serikali kupitia Wizara ya Afya nchini imeahidi kushirikiana na wadau mbalimbali wa Afya ili kuimarisha huduma za macho nchini ikiwemo utoaji wa huduma ya upasuaji mdogo, vipimo pamoja na kutoa miwani katika makundi mbalimbali ya wananchi wenye uhitaji wa huduma hizo ili kunusuru takribani wananchi milioni 6 ambao wanauwezekano wa kupata upofu wa macho.
Ameyasema hayo Juni 30, 2024 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati wa hafla ya uzinduzi wa utoaji huduma ya afya ya macho na uchangiaji fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kisasa na kuboresha miundombinu katika Taasisi ya KSI Charitable Eye Centre iliyopo Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam.

Ambapo kampuni ya mawasiliano ya Tigo Tanzania wamechangia zaidi ya milioni 351, 276, 000 katika kuhakikisha wanaunga na serikali na wadau mbalimbali wa afya ili kuendelea kuimarisha huduma za afya na kutoa huduma bora yenye kusaidia watu wenye uhitaji nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa K.S.I Charitable Eye Centre ndugu Anverali Rajpar wakati akitoa salaam za Taasisi amesema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma za upimaji wa macho pamoja na upasuaji mdogo wa mtoto wa jicho (Eye Cataract).
“Taasisi hii imekuwa ikitoa huduma hizi kwa kuweka kambi katika mikoa mbalimbali na kambi hizo zimekuwa na mafanikio makubwa kutokana na sababu kuwa huduma kutolewa kwa gharama ndogo ya Shilingi 10,000 kwa huduma zote na mtu akiwa hana kiasi hicho anahudumiwa bila malipo”. Amesema Raipar.
Ameongeza kuwa upasuaji mdogo wa kutoa mtoto wa jicho hufanyika kwa gharama ya Shilingi 50,000. ambapo katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2021 hadi 2023 jumla ya wagonjwa wa macho 35,400 walipatiwa huduma kwenye kituo hicho, kati yao wagonjwa 3,853 walifanyiwa upasuaji mdogo na wagonjwa 11,680 walipatiwa miwani ya macho.