Jeshi la Wananchi Tanzania( JWTZ) linatarajiwa kufanya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuasisiwa kwake Septemba 1, 1964 na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Julai 3, 2024 Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ ambaye pia ni msemaji wa jeshi hilo, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kwenye kamandi zote za kijeshi ikiwemo ya Jeshi la Anga, nchi kavu, Jeshi la Akiba, wanamaji (Baharini) na vikosi maalumu vya ulinzi.
Amesema yatafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani na katika maeneo hayo wananchi watashuhudia baadhi ya kazi za kijeshi hivyo wasiwe na wasiwasi na amewataka kuendelea na shughuli zao za kila siku za kiuchumi.
Amesema maadhimisho yatafunguliwa Julai 25, 2024 na kuhitimishwa Agosti 23, 2024 na kutakuwa na sherehe mbalimbali ikiwemo Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa majeshi kwa mara kwanza pia yakiambatana na mchezo wa CDF Cup.
Pia amesema maadhimisho hayo yataenda sambamba na shughuli mbalimbali za kijamii kama vile utoaji wa matibabu kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani kwa wananchi kwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano na jeshi hilo tangu kuanzishwa kwake.
“Kutakuwa na utoaji wa huduma za afya ikiwemo vipimo bure kwa wananchi, hospitali zote za Kanda za Kijeshi ikiwemo Arusha, Mwanza, Mbeya, Tabora, Zanzibar na tutatoa matibabu bure kwa wananchi ikiwemo magonjwa ya kuambukiza kama vile UKIMWI na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile shinikizo la damu, saratani ya matiti, tezi dume, sukari, maabara ya damu salama pamoja na magonjwa ya dharura, hivyo nawaomba wananchi kujitokeza kupata huduma hizi na ushauri nasaha.
“Wananchi wasiogope katika upimaji wa tezi dume ni vipimo vya damu hivyo naamini katika maadhimisho hayo watajitokeza kwa wingi waweze kujua afya zao na kupata matibabu bure.
Kutakuwa na mazoezi mbalimbali ya kivita yatakayofanyika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro hivyo niwaombe wananchi wasiwe na hofu pindi watakapoona zana za kivita ikiwemo magari, vifaru na ndege za kivita zikipita katika makazi yao.
“Niwatoe hofu wananchi wanapoona zana za kivita zinapita kwenye maeneo ya makazi yao msiwe na hofu, muendelee na shughuli zenu za kiuchumi kama kawaida kwani zana hizo zinatumika tu katika zoezi la maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi lenu ambapo mwaka huu tunataka maadhimisho haya yawe ya aina yake tofauti na miaka mingine.
“Pia tutashirikiana na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa kuwakumbuka waasisi wa majeshi haya akiwemo Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa China wa awamu hiyo, lakini pia ni kumbukumbu ya miaka sitini ya JWTZ tangu kuanzishwa kwake na pia ni kumbukumbu ya miaka sitini ya udugu na uhusiano wa mataifa haya mawili,” alisema Luteni Kanali Ilonda.
“Zoezi hili litafanyika baharini na nchi kavu hivyo litafanyika kwa uwazi ili wananchi wapate fursa ya kujionea kupitia vyombo vya habari kwa wale ambao hawapo maeneo ya baharini lakini wale ambao wapo karibu na maeneo ya baharini itakuwa fursa kwao kuona mbashara na itakuwa sehemu ya utalii kwao.
Amesema kutakuwa na utoaji huduma za matibabu bure ambapo meli ya matibabu kutoka nchini China itawasili Julai 16,2024 hivyo wananchi wote wanakaribishwa kufika kutibiwa na kutalii katika meli hiyo kwani ni fursa adhimu ambao jeshi limeandaa na maandalizi yote yameshakamilika,” amesema Luteni Kanali Ilonda.