Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, ametoa mifuko 300 ya saruji kwenye vituo viwili vinavyotoa mafundisho ya Dini ya Kiislamu ikiwemo kituo kilichopo Msikiti wa Masjid Salaf uliopo Kiluvya Madukani.
Ikumbukwe kuwa hatua hii inakuja siku kadhaa tangu aagize kituo hicho kisitishe mafunzo kwa muda na kuwarejesha watoto zaidi ya 90 kwa wazazi wao hadi watakapojenga mabweni na kupewa kibali maalum cha kuendesha mafunzo hayo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kubaini kuwa watoto hao wanalazwa katika eneo dogo msikitini na wengine nje ya msikiti huku mazingira wanayopikia chakula na yanayowazunguka yakiwa hatarishi.
Magoti ametoa mifuko 150 kwa Msikiti wa Masjid Salaf na mifuko mingine 150 kwenye Msikiti mwingine unaoitwa Masijid Abdulaziz Ashlak ambako nako walibaini Watoto wakiwa wanalala kwenye mazingira hatarishi yasiyo rafiki na kuelekeza warudishwe makwao ndani ya saa 24.

“Nimefurahi agizo limetekelezwa ndani ya saa 24, nimeamua kuchangia ujenzi na nitasaidia michakato yote ya hati ya kiwanja na usajili wa kituo,” alisema.
Kiongozi wa kituo hicho, Sheikh Abdul Hamid akiongea mbele ya Sheikh wa Mkoa wa Pwani, Sheikh Khamis Mtupa, amemshukuru DC Magoti kwa kuwachangia saruji huku akimuomba Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote walioguswa, kuwachangia kila mmoja kwa kile atakachojaaliwa ili wawezeshe kujengwa kwa bweni la ghorofa 5 na watoto warejee kuendelea na masomo.
“Tunakuomba Mama yetu (Rais Samia) kupitia hili tutulie nguvu hapa tuna injinia anahitaji milioni 26 kwa ajili kuanza ujenzi, tunakuomba mama yetu angalau tupatie hiyo milioni 26 injinia aje kuanza ujenzi na Watanzania wote tunakuombeni sana mtuchangie kwasababu Jamii haiwezi kuwa na ustaarabu bila watu kupitia kwenye mafunzo ya imani.”
Namba za kuchangia ni Tigo Pesa 0719 380 268 (Jina Abdallah Samudu).