×

Bilionea Elon Musk Atangaza Kumpa Trump Mabilioni ya Fedha Kugharamia Uchaguzi

Bilionea namba moja duniani, Elon Musk amesema kwamba anapanga kutoa takriban Dola za Kimarekani milioni 45 (sawa na takribani shilingi bilioni 119) kila mwezi kwa kamati mpya ya Super Political-Action (Super PAC) inayounga mkono jitihada za kampeni za uchaguzi za Donald Trump.

Kwa mujibu wa Jarida la Wall Street Journal, msaada wa Musk utaelekezwa kwa kundi linaloitwa America PAC, ambalo linaendesha kampeni za kumuunga mkono Trump kuwania Urais wa Marekani katika majimbo yenye ushindani mkali kabla ya uchaguzi mkuu wa Novemba.

Musk alitangaza rasmi kumuunga mkono Trump katika kampeni za urais wa Marekani Jumamosi baada ya rais huo wa zamani kunusurika kuuawa kwa risasi katika mkutano wa kisiasa huko Pennsylvania.

“Namuunga mkono kikamilifu Rais Trump na namuombea apone haraka,” aliandika Musk kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii X, ambalo alilinunua mwaka 2022 wakati likijulikana kama Twitter.

Taarifa zimeeleza kuwa Musk anapanga kuanza kutoa michango mwezi ujao na inaelezwa kuwa amekuwa na urafiki wa karibu na Trump katika kipindi hiki cha vuguvugu la kuelekea uchaguzi wa Marekani wa 2024.

Mwezi Machi, wawili hao walikutana ana kwa ana wakati wa hafla ya kifungua kinywa cha wafadhili kilichofanyika katika makazi ya bilionea Nelson Peltz huko Florida.

Ingawa michango ya kampeni ya mtu binafsi nchini Marekani imewekewa kiwango cha juu cha dola za Kimarekani 3,300 kwa kila mtu, mianya katika mfumo wa fedha za kampeni wa Marekani inaruhusu wafadhili wakubwa wa kisiasa kuchangia kwenye fedha zinazojulikana kama kamati za utekelezaji wa kisiasa, zinazojulikana zaidi kama “PACs,” ambazo zinaunga mkono wagombea.

America PAC imeajiri mamia ya wafanyakazi kwa ajili ya juhudi zake za kumuweka Trump madarakani, na imekuwa ikisajili wapiga kura, kuzungumza na wapiga kura katika majimbo yenye ushindani.

Leave a Comment