
MBUNGE wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika akiwa katika ziara Kata ya Kifanya amewapongeza wananchi wa vijiji vya Kifanya, Utengule na Lwangu kwa kuchangia na kuendeleza shughuli mbalimbali za ujenzi katika vijiji vyao kama ujenzi wa shule shikizi kitongoji cha Itengule – Kifanya, shule shikizi Mzalendo – Lwangu na ujenzi wa nyumba ya Mtendaji kijiji cha Utengule.
Mhe. Mwanyika amewachangia tripu 10 za mawe ujenzi wa shule shikizi Itengule zenye thamani ya Sh. 1,300,000, saruji mifuko 30 (Sh. 555,000) ujenzi wa nyumba ya Mtendaji Kijiji cha Utengule, saruji mifuko 20 (Sh. 370,000) ujenzi wa shule shikizi Mzalendo – Lwangu ambapo ametoa kupitia mfuko wake binafsi.

Pia ametoa tenki la maji shule ya Msingi Msindu lenye thamani ya (Sh. 2,000,000) na saruji mifuko 30 (Sh. 555,000) shule shikizi Mzalendo – Lwangu ambazo fedha hizo zitatolewa kupitia Mfuko wa jimbo.
Mwanyika amewaasa wananchi kuendelea na moyo wa kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo, na serikali itaendelea kutoa fedha katika ujenzi huo.

Serikali imeendelea kuunga mkono juhudi za wananchi kwa kutoa fedha katika Sekta ya Elimu, Afya, Kilimo, Maji, Barabara na Umeme ikiwa lengo kuu ni kumsogezea huduma bora mwananchi katika maeneo yao.
Mwanyika ameanza ziara jimboni kwake yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuhakiki taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba mwaka huu, pamoja na kuhuisha uhai wa chama.
