
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Abdulamjid Nsekela amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuizindua Benki ya Taifa ya Ushirika Tanzania kwani maandalizi yote muhimu yamekamilika.
Nsekela ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB pia, ametoa ombi hilo leo, tarehe 10 Agosti 2024, kwenye mkutano ulioitishwa na Rais Samia kumkutanisha na maafisa ugani pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika kutoka halmashauri zote nchini.

Kwenye mkutano huo uliofanyika katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Nsekela amesema TCDC imekamilisha utaratibu unaohitajika kisheria na Benki Kuu ya Tanzani (BoT) imeshatoa leseni ya kuanzishwa kwa Benki hiyo ya Taifa ya Ushirika Tanzania.

“Mheshimiwa Rais, matarajio ni kuizindua benki hii mwishoni mwa mwezi Septemba 2024 ili kuanza shughuli zake. Na, tumeomba kupitia Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo kuwa, wewe Mheshimiwa Rais, uwe mgeni rasmi katika tukio hilo muhimu,” amesema Nsekela.
Ili kukamilisha mahitaji ya kimtaji ya Benki ya Taifa ya Ushirika Tanzania, Rais Samia ametoa shilingi bilioni 5 kuvichangia vyama vya ushirika kumiliza asimilia 51 ya hisa katika benki hiyo mpya.