
MAWAZO chanya ya utajiri daima hukaa kwa mtu mwenye kiu ya mafanikio. Kila kunapokucha ataendelea kuwaza afanye nini ili awe mwenye mafanikio kwenye maisha yake.
Siri ya utajiri wa kweli ipo kwenye ujasiriamali. Huo ndiyo ukweli ambao wengi hawapendi kuusikia. Hawapendi kwa sababu ni maisha ya kubahatisha. Mjasiriamali ni mtu aliyejitolea kupambania maisha yake kufa na kupona.
Ni mtu aliyeamua kufanya biashara hata kwa kuanza kwa kudunduliza, akiwa hana uhakika wa kupata faida au hasara. Akiwa hana uhakika wa mshahara kama mwajiriwa. Mtu huyu hana uhakika wa bima ya afya wala kiinua mgongo kwa sababu hajaajiriwa mahali popote.
Mjasiriamali hupambana usiku na mchana katika mradi wake, ili siku moja awe mwenye mafanikio. Hakuna msamiati wa kushindwa kwa mjasiriamali, bali kuna kubadilisha mbinu. Leo akipata hasara, anachofanya ni kubadilisha mbinu.
Ukweli ni kwamba si wote wanaweza kuwa wajasiriamali, lakini pamoja na ukweli huo, kwa mwajiriwa ni vigumu sana kuwa mwenye mafanikio kwa kutegemea mshahara pekee, labda awe kwenye nafasi kubwa na mshahara mkubwa kazini.
Lakini sote tunajua kuwa, asilimia zaidi ya 70 ya waajiriwa ni wale wenye nafasi za kawaida na hulipwa mishahara ya kawaida ambayo wengine huwa haiwatoshi kwa mahitaji yao ya muhimu.
Ni asimilia takribani 15 tu ya waajiriwa wengi huwa mabosi kwenye ofisi zao na hivyo kuwa na uhakika wa kupata mishahara mikubwa ambayo huwawezesha kuishi maisha wanayotaka na kupanga mipango yao mbalimbali.
Kwa msingi huo, ili mtu aweze kufanikiwa au kujiwekea mizizi ya maisha bora hapo baadaye lazima awekeze mapema. Uwekezaji wake hauwezi kuwa wenye msaada mkubwa kwa kutegemea mshahara tu!
Kamwe hilo haliwezekani. Kutegemea mshahara pekee, mwisho wake ndiyo pale mtu anapostaafu na kupewa kiinua mgongo chake, anaposhindwa kumiliki fedha zake na kuziendeleza na mwisho wake anafilisika na kuanza kupambana na ugumu wa maisha ya uzeeni.
Kutokana na hayo basi ni sahihi ikiwa mtu atajitahidi kufanya ujasiriamali hata kama ameajiriwa. Malengo makuu ni kuwekeza, lakini pia kujizoesha kumiliki fedha na kuendesha biashara.
Hii humkomaza mtu hata ikitokea amestaafu au kufukuzwa kazi, isiwe tatizo kwake kwani atakuwa na kitu kingine anachokitegemea.
Hata hivyo, swali kuu kwa waajiriwa wengi ni je, ni biashara gani naweza kuifanya na isiingilie kazi ya mwajiri wangu? Ni swali zuri kwa hakika, maana kama umeajiriwa, tunatazamia ufanye kazi kwa bidii, bila kuiba muda wa mwajiri wako na kwa hakika juhudi yako kazini ndiyo hakikisho na kibarua chako.
Je, ni biashara gani zinawezwa kufanywa na mwajiriwa bila kuathiri ajira yake na akafanya kwa ufanisi na kumwingizia fedha? Tutaona hapa chini.
Huduma za kifedha siku hizi zimekuwa na uhakika mkubwa wa kutengeneza fedha. Mradi huu hautakuhitaji uwepo kazini hapo, badala yake unaweza kumuajiri mtu. Pia mradi huu ni vigumu kuibiwa hesabu maana kila kitu hubaki kwenye elektroniki.
Kutoa huduma ya fedha kupitia mitandao, uuzaji wa umeme, vocha, nishani mbadala na miamala ya kampuni mbalimbali ni biashara ya uhakika. Cha muhimu ni kupata ushauri kwa mtu mwenye uzoefu wa kutosha na kazi hii.
Baada ya hapo ni kuwa na mtaji na mahali pa kufungua mradi wako ambapo lazima kuwe na mwingiano/mzunguko wa watu wengi kulingana na mradi wenyewe kuhitaji pilika za watu.
Bahati nzuri makampuni mengi huwadhamini wafanyakazi wake mikopo, kwahiyo una uwezekano mkubwa wa kuchukua mkopo kutoka benki kwa dhamana ya kampuni unayofanyia kazi na mara moja ukaanzisha mradi wako ambao utakuhakikishia fedha na wakati huohuo ukiendelea kuvuta mshahara wako kila mwezi.
Kumbuka, biashara yako itaendelea huku nawe ukiendelea na ajira yako bila kuharibu kazi yako kwa kuwa haziingiliani.
HUDUMA ZA USAFIRI
Biashara ya usafiri, ukiacha kujiweka kwenye risk ni mradi mzuri unaoweza kukuingizia fedha. Mfano ukiweza kuanza japo na bodaboda mbili na kuwapa vijana wafanyie kazi, zinaweza kukulipa.
Ili kujiepusha na ujanja wa namna yoyote, inashauriwa kuingia mkataba na dereva wako – awe anakupatia labda shilingi 10,000 kila siku au 70,000 kila wiki au 300,000 kwa mwezi kwa muda mtakaokubaliana, ili akimaliza pikipiki iwe yake.
Wengi huwekeana makubaliano ya shilingi milioni 3, ambapo hulipwa kwa miezi kumi. Mathalani pikipiki umenunua kwa Tsh. 2 milioni, hapo kuna faida ya uhakika ya 1 milioni ndani ya miezi kumi, hiyo humaanisha kuwa kwa mwezi una uhakika wa kuingia 100,000 huku ukiendelea na ajira yako.
Vipi ukiwa na pikipiki tatu au tano kwa wakati mmoja? Mbali na bodaboda, hata Bajaj unaweza kumkabidhi mtu na ukatengeneza fedha ukiwa upo kazini kwako. Ni vile tu wengi huwa hatuumizi kichwa na kubaki kusubiria mshahara usome kwenye akaunti mwisho wa mwezi.
HUDUMA ZA CHAKULA
Huduma za chakula pia ni biashara nzuri. Fanya utafiti, tafuta mpishi mzuri kisha fungua mgahawa. Mbali na mgahawa, unaweza kutafuta oda kwenye ofisi mbalimbali na ukawa unahudumia chakula kila siku mchana.
Kuna wanaokwenda mbali zaidi, huingia mkataba na kampuni kulisha wafanyakazi kwa mwezi mzima, kisha kulipwa fedha zao mwisho wa mwezi (na kampuni kama mdhamini wa wafanyakazi).
Tafiti zinaonyesha kuwa, biashara ya chakula pekee ndiyo biashara isiyochuja – ni kipaumbele kwa kila binadamu, bila kujali uwezo wa fedha.
SALUNI
Biashara ya saluni ya kike au kiume, haikuhitaji uwepo kazini. Uzuri wa biashara hii huweza kukubaliana malipo na ukawa unapewa fedha yako mwisho wa wiki na kuwaacha wafanyakazi wakiendelea na majukumu yao kwa uhuru.
DUKA LA MAVAZI
Duka la mavazi ni biashara nzuri ambayo unaweza kupanga bei na kumuacha mfanyakazi akiiendesha bila matatizo. Uzuri wa biashara hii unaweza kuifanya hata mwenyewe kazini kwako kwa wafanyakazi wenzako.
Kwa kuwa ni watu unaofahamiana nao, unaweza kutoa hata kwa mkopo na ukawa unachukua fedha mwisho wa mwezi baada ya mshahara kutoka.
FAIDA UTAKAZOPATA
Faida kubwa ni kujikomaza kibiashara. Unakuwa unaujua ujasiriamali mapema na nidhamu ya fedha. Kwa kawaida mwajiriwa hana nidhamu ya fedha kwa kuwa anajua mwisho wa mwezi pesa yake ipo.
Kumbuka kuna kustaafu. Hakutakuwa na jipya kwako, kwa sababu tayari umeshajiwekea misingi ya kijasiriamali na utakuwa na akiba yako ya kutosha, hivyo ukipewa mafao yako ya uzeeni inakuwa rahisi kuendesha miradi na kufurahia uzee wako.
Mafanikio hayajengwi kwa siku moja. Ni hatua.
Zaidi nifuate kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii, Facebook: simulizi za shaluwa, Instagram: @joeshaluwa