Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), wametoa mafunzo kwa waandishi wa habari zaidi ya 50, ambao ni wanachama wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari nchini (JOWUTA) kwa lengo la kujengewa uelewa kuhusu usalama kazini.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika Ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo waandishi hao wamehamasishwa kuwa daraja la kufikisha elimu waliyoipata kwa wananchi ambao wengi wao hawajui kazi zinazofanywa na OSHA.
Pia wameelezwa namna ya kutambua vihatarishi vya mahala pa kazi sambamba na sheria zinazofuatwa na OSHA katika kutekeleza majukumu yao yakiwemo ya kuhakikisha kunakuwepo na afya na usalama wa wafanyakazi mahali pa kazi.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa OSHA, Hadija Mwenda amesema wameona ni vyema wakakutana na JOWUTA kwa ajili ya kupeana elimu kuhusu usalama mahala pa kazi.
“Tumefanya tathimini na kubaini uelewa kwa jamii kuhusu usalama mahala pa kazi ni mdogo, hivyo tumeona tuwashirikishe waandishi wa habari ili wasaidie kutoa elimu kwa wananchi,” alisema.
“Ni ukweli kwamba hakuna mazingira ya kazi ambayo hayana vihatarishi, tunataka mtu akistaafu asione ndiyo anakwenda kufa, kumekuwa na magonjwa ya misuli, shingo, mgongo ambayo ndiyo yanaitafuna dunia na ili tuondoe magonjwa hayo, lazima tutoe elimu kuhusu mtindo wa maisha sehemu za kazi.
“Matarajio yetu elimu ambayo mtaipata mtaifikisha kwa Watanzania. Watu lazima wajilinde na kujilinda ni pamoja na watu kupata elimu, tunafahanu Tanzania ina watu zaidi ya milioni 60 lakini tukiwafikisha waaandishi 400 ambao ni wanachama wa JOWUTA maana yake nao watawafikia mamilioni ya Watanzania,” amesisitiza.
Mkurugenzi huyo amesema waandishi wamekuwa wakienda katika maeneo mbalimbali katika kufanya kazi zao na wakati mwingine hukutana na mazingira hatarishi kama maeneo ya migodini na viwandani hivyo ni muhimu wapitie mafunzo hayo ili yawasaidie kutambua vihatarishi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma amesema wanaishukuru OSHA kwa kukubali kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ambao ni wanachama wao na matarajio yao ni kuona mafunzo hayo yanakuwa endelevu.
Amesema waandishi wanakutana na changamoto nyingi katika kuteekeleza majukumu yao, hivyo endapo OSHA wataendelea kuwajengea uelewa itapunguza baadhi ya changamoto hizo.
Awali, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleiman Msuya amesema JOWUTA inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na ina jumla ya wanachama 400 nchi nzima na leo wanachama wake 50 ndio wanapatiwa mafunzo hayo na maombi yao kwa OSHA ni kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa wanachama wao walioko mikoani.
“Kwa Dar es Salaam tunao wanachama zaidi ya 80 lakini tuliona katika mafunzo hayo tuwe na washiriki 50 kutoka Dar es Salaam na Pwani, tunaamini mafunzo haya ni muhimu kwa wanachama wetu, amesema,” Msuya.
Stori: Sabina Wandiba