
Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Viwanja vya Ndege Tanzania wa Mwaka 2024 ambapo ukisainiwa na Rais utaanzisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) itakayosimamia, kuendesha na kuendeleza wa viwanja vya ndege.
Waziri wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa amesema katika taarifa yake Bungeni kuwa kusudio la sheria hiyo ni kuweka mfumo madhubuti na thabiti wa kisheria wa Usimamizi, Uendeshaji na Uendelezaji wa viwanja vya ndege nchini.
“Sheria hii inafuta Sheria ya Utoaji wa Leseni na Udhibiti wa Viwanja vya Ndege ya mwaka 1974. Kwa mujibu wa masharti ya Muswada, Mamlaka inayopendekezwa kuanzishwa itaendelea kutekeleza majukumu yake kama Mamlaka,” amesema Prof Mbarawa.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania imekuwa ikikumbana na changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake. Muswada huo mbali na kuanzisha mamlaka unaanzisha Bodi ya Wakurugenzi, mamlaka ya Bodi, uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu na masuala mengine yanayohusu maafisa na watumishi wa Mamlaka.
“Mamlaka inapendekezwa kupewa jukumu la kuanzisha rejista ya taarifa za viwanja vya ndege na kuanzisha kamati mbalimbali katika kila kiwanja cha ndege kwa lengo la kutekeleza na kuwezesha shughuli za viwanja vya ndege,” amesema. Pia Mamlaka itaweka ada na tozo za huduma mbalimbali za viwanja vya ndege, kufuatilia maeneo ya vizuizi vya viwanja vya ndege kwa kufanya ufuatiliaji na ukaguzi kwenye maeneo ambayo yako karibu na viwanja vya ndege.