
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amekanusha taarifa ya kufanyika kwa kikao cha viongozi wa chama hicho kupanga maandamano kupitia mtandao wa Zoom, huku akilitaka Jeshi la Polisi kutoa ushahidi wa kikao hicho.
Mbowe amesema hayo kufuatia taarifa ya Polisi iliyotolewa leo Agosti 30, 2024 na Msemaji wake David Misime kuwa viogozi wa chama hicho wamepanga kuandamana nchi nzima na kuvamia vituo vya polisi.
“Ni mkakati wa Jeshi la Polisi kutafuta kisingizio cha kukamata na kutesa Wanachadema kwa taarifa toka vyanzo vya uongo. Waeleze hicho Kikao cha Zoom kilifanyiwa na akina nani” amesema Mbowe katika ukurasa wake wa X
Kwa mujibu wa Misime, hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi wa kutoweka kwa baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deusdedit Soka, Jacob Godwin Mlay and Frank Mbise.
Misime amesema Chadema katika kikao hicho walikubaliana kuanza kuhamasisha wafuasi wao chini chini kufanya maandamano ya kuelekea maeneo tofauti zikiwepo ofisi mbalimbali.
