
Wizara, Taasisi, Mashirika, wakala za Serikali zimetakiwa kutenga Bajeti ya kutosha kwa ajili ya kushiriki Michezo ya SHIMIWI ili kukidhi malengo na misingi ya kuanzishwa kwa kwa michezo hiyo na kuleta tija.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua mshindano ya 38 ya SHIMIWI Yanayoendelewa Mkoani Morogoro ambapo amesema hatopenda kusikia visingizio vya aina yoyote kutoka kwa wale wasiotuma washiriki.
“Kama tumekubaliana kufanya jambo lazima tulifanye jambo linakuwa ni lazima siyo hiari, Kama kuna sababu ya kuliboresha tuboreshe kwa kufanya mabadiliko na siyo kukubaliana bila kufanya utekelezaji” amesema Dkt. Biteko na kuongeza kuwa michezo hiyo inafanyika kwa mujibu wa sheria na kama kuna changamoto zibainishwe na kufanyiwa marekebisho.

Agizo la Dkt. Biteko linafuatia kushuka kwa idadi ya vilabu vinavyoshiriki mashindano hayo kutoka 74 mwaka 2023 hadi 66 mwaka 2024 jambo ambalo amesema linaashiria uwepo wa changamoto katika uendeshaji wa michezo ya SHIMIWI na hivyo kuwaagiza waajiri na Wakuu wa Taasisi ambao hawakutuma washiriki kutoa maelezo juu ya uamuzi wao kwa ajili ya hatua siku zijazo.

Dkt. Biteko pia amewataka watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa watanzania bila kuzingatia tofauti zao, kuzingatia matumizi ya TEHAMA, Ushirikishaji wa Serikali na sekta binafsi katika kuelekea maendeleo ya pamoja na kuzingatia Utawala wa Sheria, taratibu pamoja na kushirikisha makundi ya watu wenye mahitaji maalum.
Amesema Mashindano ya aina hiyo mbali na kuwauganisha watumishi, lakini yanawezesha mshikamano miongoni mwao na kujenga afya ambayo ndio msingi watendaji bora wa kazi na wenye tija.