
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya ahakikishe mkandarasi anayejenga mabweni, madarasa na vyoo katika shule ya sekondari Mandawa awe ameanza kazi ifikapo Oktoba 24, mwaka huu.
Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo pamoja na viongozi wa Wilaya hiyo, Oktoba 21, 2024 mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeamua kuipandisha hadhi shule hiyo kwa kuamua kuifanya iwe na madarasa ya kidato cha tano na sita.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, yupo wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku nne, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa sh. milioni 545 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni matatu, madarasa sita na matundu ya vyoo 12 katika shule hiyo, iliyopo kata ya Mandawa, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
