
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kumalizika kwa mkataba wa ununuzi wa umeme kutoka Kampuni ya uzalishaji umeme kwa njia ya Gesi asilia ya Songas. Mkataba huu umedumu kwa muda wa miaka ishirini (20) na umefikia ukomo wake tarehe 31 Oktoba 2024.
Taarifa ya Novemba 1, 2024 iliyotolewa na TANESCO imebainisha kuwa pamoja na kufika ukomo wa mkataba huo Shirika hilo limewahakikisha wateja wake kuwa hali ya upatikanaji wa umeme nchini ni nzuri kwa kuzingatia vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme ambapo kwa sasa uwezo wa uzalishaji umeme kwa kutumia mitambo ya Gesi asilia na mitambo inayotumia maji ni mkubwa kuliko mahitaji ya umeme hapa nchini.
“Hali hii imechangiwa na maendeleo mazuri ya Mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo mpaka sasa jumla ya megawati 940 zimeungwa kwenye Gridi ya Taifa.” — TANESCO
“Maamuzi ya Serikali kutokuendelea na mkataba huu ni kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya nchi. Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO itaendelea kusimamia sekta ndogo ya umeme ili kuhakikisha kunakuwa na huduma bora, endelevu na ya uhakika ya umeme.” — imesema TANESCO
