
Mgombea urais kupitia chama Cha Republican, Donald Trump (78), ameshinda kiti Cha urais nchini Marekani na kuwa Rais wa 47 wa Taifa hilo, akimzidi mpinzani wake Kamala Harris kutoka chama Cha Democratic ambaye pia ni Makamu wa Rais wa sasa.
Trump ameshinda kiti hicho Kwa jumla ya kura za wajumbe (electoral vote) 277 dhidi ya kura 224 za Kamala Harris, huku katika jumla ya kura zote Trump amejikusanyia kura Milioni 70 ambazo ni sawa na asilimia 51 dhidi ya kura Milioni 65 ambazo ni sawa na asilimia 47.
Trump anarejea tena katika kiti hicho baada ya kuongoza katika awamu ya kwanza mwaka 2016-2020, na kisha kushindwa katika awamu ya pili dhidi ya Rais wa Sasa Joe Biden, hivyo Trump atashikilia nafasi hiyo kubwa ya uongozi na yenye heshima kubwa nchini Marekani Kwa miaka minne ijayo, ambapo ataapishwa rasmi kuwa Rais mapema januari 20 mwakani.
Donald John Trump alizaliwa Juni 14, 1946, huko Queens New York nchini Marekani, na kisha kupokea shahada ya Sayansi ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania mwaka 1968. Lakini pia baba yake alimfanya rais wa biashara ya mali isiyohamishika ya familia mwaka 1971.
Trump alifanikiwa kushinda uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 akiwa na chama chake cha Republican dhidi ya mgombea wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton na kufanikiwa kuliongoza Taifa hilo akiwa Rasi wa 45.
Katika awamu yake ya kwanza, Trump alihamisha fedha za kijeshi ili kujenga ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico, lakini pia alisaini sheria ya kupunguza kodi ya 2017 (Tax Cuts and Jobs Act), ambayo ilipunguza kodi na kuondoa adhabu ya bima ya afya kwa mtu binafsi katika Sheria ya Huduma Nafuu ya Afya (Affordable Care Act).
Na Sasa Donald Trump amerejea Tena katika kiti hicho, huku miongoni mwa vitu alivyopanga kuvisimamia ni kupunguza wahamiaji haramu nchini humo.