
DESEMBA 25 kila mwaka, Wakristo ulimwenguni kote usheherekea maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.
Sherehe hizo maarufu kwa jina la Krismasi huwaleta pamoja ndugu, jamaa na marafiki kukaa pamoja kwa kula na kunywa huku wakipeana zawadi mbalimbali.
Katika kuadhimisha sikukuu hiyo kwa mwaka huu, Kwaya Flying Family inayojumuisha waimbaji kutoka madhehebu mbalimbali ya kikristo wenye vipaji vya uimbaji wameamua kuendelea kuwa sehemu ya zawadi ya msimu wa sikukuu kwa kuwakutanisha wana wa Mungu na familia zao kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji wa nyimbo zenye ufundi wa hali ya juu.
Kwaya inajivunia kujenga umoja na upendo kwa wakristu kwa kutumia muziki na kuweza kuimba pamoja bila kujali tofauti zao za kimadhehebu kwa kipindi cha miaka sita sasa na kufanikiwa kuandaa matamasha makubwa saba yaliyowakusanya waumini na viongozi mbalimbali wa kidini na kiserikali chini ya mchungaji mmoja Yesu Kristo.

Kwaya hiyo itafanya tamasha kubwa na wanakwaya wake kuimba ‘Classical music’ ambao ni maarufu duniani kote na umejizolea umaarufu tangu miaka ya zamani.
Innocent Fundisha ni Kiongozi wa kwaya hiyo anasema wapenzi wa muziki mtakatifu wakifika katika tamasha hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Desemba 15, mwaka huu katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jiini Dar es salaam watapata kusikia kazi za watunzi nguli kama George Handel, Wolfgang Mozart, Johan Bach, Joseph Haydn, Felix Mendelson, Anthonio Vivald na wengine wengi.
Hata hivyo anasema pia wanatumia kazi za watunzi wazawa kama David Wasonga, John Mgandu, Egidius Mushumbusi na Mathias Msafiri bila kusahau tenzi za rohoni.
Anasema tiketi za tamasha hilo zinapatikana Kanisa Katoliki la St Peter Osterbay, Kanisa la Kiinjili na Kilutheri (KKKT) Msasani, Ofisi za Paones Posta Samora tower, KKKT Goba, Kanisa Katoliki Mwenge na Kanisa la Anglican Ilala. Kiingilio kitakuwa Sh. 50,000 kwa wakubwa, 30,000 kwa Watoto na 100,000 kwa VIP.
Pamoja na muziki mzuri siku hiyo kutakuwa na chakula na vinywaji vya kutosha kwa washiriki wote kama sehemu ya shangwe za msimu wa sikukuu.
Fundisha anasema si kazi rahisi kwa wanakwaya kujifunza nyimbo hizo lakini kwa msaada wa Mungu wanafanikiwa kushika na kujifunza kwa usahihi.
“Kwaya hii ilianzishwa Aprili, 2018 jijini Dar es Salaam ikiwa na wanakwaya wasiozidi 15 ila kwa sasa ina wanachama hai 40, tumeamua kumsifu Mungu na kutangaza sifa zake hapa duniani kwa njia ya uimbaji na kutumia muziki kudumisha umoja wa madhehebu ya kikristu,” anasema Fundisha.
Anasema anatambua kuwa sikukuu ya Krisimasi huwaleta pamoja na ndugu, jamaa na marafiki hivyo anaamini kupitia tamasha hilo watu wataburudika, watafurahi na kudumisha utamaduni wa kusheherekea Krismasi kwa njia ya muziki wa classical.
“Tunatarajia kuwa na Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo Kuu la Dar es Salaam, Thaddaeus Ruwai’chi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, Askofu Jackson Sosthenes wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Dar es salaam.
“Pia tutakuwa na maaskofu wasaidizi Stephano Musomba na Henry Mchamungu wa Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam, mapadre na wachungaji. pamoja nao tutakuwa na ushiriki wa viongozi wa serikali pamoja na viongozi wastaafu, wanadisplomasia wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, wakuu wa mashirika na taasisi za kiserikali na binafsi pamoja na washiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania,” anasema
Lengo la kwaya hiyo ni kuleta umoja na mahusiano mazuri katika madhehebu ya kikristo kwa njia ya kushirikishana vipaji vya kimuziki.
“Tunashirikishana vipaji hivyo vilivyopo kwa kuandaa kwaya ya pamoja, matamasha mbalimbali, huduma kwa wahita…