×

Jeshi la Polisi: Nondo Alitelekezwa Coco Beach, Uchunguzi Unaendelea

Jeshi la Polisi Tanzania limesema Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama cha ACT- Wazalendo, Abdul Nondo ambaye alikamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu wasiojulikana katika eneo la stendi ya Magufuli Mbezi Louis Dar es Salaam jana Disemba 1, 2024 majira ya asubuhi alitelekezwa jana usiku katika fukwe za Coco.

Taarifa ya leo Desemba 2, 2024 iliyotolewa msemaji wa jeshi la Polisi DCP David A. Misime imeeleza kuwa baada ya kutelekezwa katika fukwe hizo, aliomba msaada wa bodaboda kumfikisha katika ofisi za chama chake Magomeni, Dar es Salaam.

“Desemba mosi, 2024 majira kama saa nne na nusu usiku Abdul Omary Nondo ambaye tulikuwa tunamtafuta kwa kushirikiana na watu mbalimbali, wakiwepo viongozi wake wa chama cha ACT Wazalendo baada ya kukamatwa na kuchukuliwa kwa nguvu pale kituo cha mabasi cha Magufulli, ameeleza alitelekezwa maeneo ya fukwe za Coco (Coco Beach) Kinondoni, Jijini Dar es Salaam na watu asiowafahamu.” imesema taarifa hiyo

“Baada ya kutelekezwa alisimamisha bodaboda na kumwelekeza amfikishe katika ofisi za chama chake zilizopo Magomeni, Jijini Dar es Salaam na walifika muda wa saa tano usiku,” imeeleza tarifa hiyo na kuongeza kuwa alionana na viongozi wake na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

Leave a Comment