Waziri Mkumbo Atangaza Mchakato Wa Maandalizi Ya Dira Ya Taifa Ya Maendeleo 2050

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ametangaza hatua za mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akibainisha kuwa tayari timu yake imeshakamilisha rasimu ya kwanza ya dira hiyo.
Akizungumza katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Ijumaa tarehe 6 Disemba 2024, Profesa Kitila rasimu hiyo imejumuisha hatua mbalimbali na maoni mseto ya wananchi nchi nzima.
“Tunayo sasa rasimu ya kwanza. Hatua inayofuata ni kuzinduliwa kwa rasimu hii, lakini tukishazindua siyo mwisho.” Amesema Prof. Kitila.
Ameeleza kuwa baada ya kuzinduliwa kwa rasimu hiyo, mchakato utaingia awamu ya pili ya ukusanyaji wa maoni ya ziada kutoka kwa wadau kupitia hatua inayojulikana kama uhakiki, ambapo rasimu hiyo itasambazwa kwa wananchi kupitia mitandao na vyanzo vingine ili waweze kusoma na kutoa maoni maalum.
“Safari hii maoni hayatakuwa ya jumla bali maalumu. Wananchi watakabidhiwa rasimu na maudhui yaliyojitokeza, kisha wataulizwa, ‘hivi ndivyo tunavyopendekeza, una maoni gani? Tuboreshe wapi?’ Baada ya hapo itaandaliwa rasimu ya pili.” Amesema.
Profesa Kitila amebainisha kuwa hatua ya itakayofuata ya mchakato huo ni kuzinduliwa kwa Rasimu ya Pili ya Dira na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, tarehe 18 Januari 2025, na kuhitimisha mchakato wa wananchi kabla ya kuendelea na hatua nyingine ili kukamilishwa kuandikwa kwa dira yenyewe.
“Rasimu ya Pili itajumuisha maoni yote ya wadau yaliyokusanywa katika hatua ya uhakiki. Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha kwamba Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inakuwa mchakato wa wananchi.” Ameongeza Prof. Kitila

