Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kushiriki Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal AlD Campaign, yenye lengo la kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
Kampeni hiyo itasaidia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini.
Wito huo umetolewa leo Desemba 12 na mkuu huyo wa wilaya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Adam Malima wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake na kuweka bayana kuwa uzinduzi wa kampeni hiyo utazinduliwa rasmi kesho Desemba 13, 2024 katika viwanja vya stendi ya zamani ya daladala iliyopo katika Manispaa ya Morogoro kuanzia kuanzia saa 2:00 asubuhi, huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro.
Kilakala amesema kampeni hiyo inatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji wa haki, mifumo ya utoaji haki, kuweka mazingira wezeshi ya kulinda na kukuza haki ya upatikanaji haki kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini.
“Naomba kutoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro kushiriki uzinduzi huo ili kupata Elimu ya msaada wa kisheria tuweze kuzitatua kero na migogoro iliyopo bila ya malipo yoyote…” amesisitiza Mussa Kilakala.
Aidha, amesema mara baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo kukamilika, utekelezaji utaendelea katika Halmashauri zote 9 za Mkoa wa Morogoro na kila Halmashauri itafikiwa na huduma hiyo ndani ya Kata 10 na Vijiji 30 hivyo amewasisitiza wananchi kushiriki kwa wingi katika kampeni hizo katika kata zao ni vijiji au mitaa yao, lengo likiwa ni kukamilisha ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuwapatia haki ya msingi wananchi walio wanyonge.
Kampeni hiyo katika Mkoa wa Morogoro ambayo imejikita katika kuto elimu ya masuala ya kisheria itafanyika ndani ya siku 9.