
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo Wilaya ya Magu.
Amesema hayo Desemba 23, 2024 wilayani Magu mkoani Mwanza katika Mkutano Mkuu Maalum ambapo taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu Jimbo la Magu kwa mwaka 2020 hadi 2024 iliwasilishwa.

“Mhe. Rais amefanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano na anastahili pongezi, nataka niwaambieni kuna watu wengine wanaumia tukimpongeza Rais Samia, lakini wajue hatutoi pongezi hizi peke yetu hata huko duniani kwa mfano Benki ya Dunia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanampongeza kwa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa asilimia 5.1,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema pia kuwa Rais Samia ana nia njema na anataka kuona Watanzania wanapata maendeleo.
Ameongeza kuwa maendeleo katika Jimbo la Magu hayakuja kwa bahati mbaya isipokuwa kwa mipango na hivyo anawapongeza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Magu kwa tamko la pongezi kwa Rais Samia kwa kuwapa fedha kiasi cha shilingi 143.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Ametaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa na Serikali “ Barabara za lami zimeunganisha mikoa yote nchi nzima, tuna ndege za abiria na mizigo, tumejenga shule nyingi na sasa tunajenga shule za kata maeneo mbalimbali nchini. Maendeleo yanaonekana kwa macho na sisi ni kazi yetu kusema haya kwa wivu mkubwa,”
Kuhusu umeme Dkt. Biteko amesema katika kijiji kimoja pekee ambacho hakina umeme, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya kupeleka umeme huku mipango ya kupeleka umeme katika kisiwa ikiendelea.

Aidha, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Magu, Mhe. Kiswaga kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
Dkt. Biteko amesema “CCM ni chama kiongozi hivyo wanaCCM tembeeni kifua mbele hubirini yanayofanywa na chama chenu waonesheni watu maendeleo yaliyotokea msiwapuuze,”