×

Malawi yaamuru wanajeshi wake kujiandaa kuondoka mashariki mwa Kongo

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ameviagiza vikosi vya ulinzi kuanza kujiandaa kuwaondoa wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano.

Wanajeshi hao wa Malawi ni sehemu ya kikosi cha wanajeshi kutoka jumuiya ya kanda ya kusini mwa Afrika waliotumwa nchini Kongo kuisaidia kupambana na waasi wenye silaha. SADC iliongeza muda wa misheni ya kijeshi mwishoni mwa mwaka jana.

“Rais Chakwera amemuagiza Kamanda wa MDF (Jeshi la Ulinzi la Malawi) kuanza maandalizi ya kuwaondoa wanajeshi wa Malawi… kuheshimu tamko la pande zinazozozana kusitisha mapigano na kuandaa njia ya mazungumzo yaliyopangwa kwa ajili ya kuleta amani ya kudumu,” imesema taarifa hiyo.

Muungano wa waasi, unaojumuisha wapiganaji wa M23, ulitangaza kusitisha mapigano kwa sababu za kibinadamu kuanzia siku ya Jumanne.

Mapigano yameanza tena katika mkoa jirani wa Kivu Kusini. Na duru za kuaminika zinasema kuwa waasi wa M23 wamechukuwa udhibiti wa mji wa uchimbaji madini wa Nyabibwe, yapata kilomita 100 kutoka Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini.