
NAIBU Waziri Mkuu na ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dr. Doto Biteko anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika mbio za kimataifa za Kilimanjaro International Marathon ambazo zinaingia msimu wake wa 23 mwaka huu.
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 23, mwaka huu, katika uwanja wa chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCU) kilichoko Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji wa Kilimanjaro International Marathon, Naibu Waziri Mkuu amethibitisha kushiriki na kwamba ataambatana na viongozi wengine wa kitaifa na wale wa ngazi ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Naibu Waziri Mkuu anatarajiwa kuzindua mbio za kilomita 42, zile za kilomita 21 maarufu kama Yas Kili Half Marathon na baadaye kushiriki mbio za kilomita 5 maarufu kama CRDB 5 km Fun Run”, ilisema taarifa hiyo ya waandaaji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mbio hizo zitatanguliwa na maonyesho ya Kili Expo ambayo yatafanyika kwa mara ya nne mwaka huu, ambapo yanatarajiwa kuwakutanisha wadhamini wa mbio hizo pamoja na wafanyabiashara mbalimbali.
“Maonyesho hayo ambayo yanatarjiwa kufanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Ijumaa Februari 21, mwaka huu, yatahusisha bidhaa aina mbalimbali pamoja huduma ambazo zinatolewa na wadhamini hao pamoja na wafanyabiashara wengine watakaoshiriki”, iliendelea kusema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa maonyesho hayo yataenda sambamba na zoezi la uchukuaji wa nambari za ushiriki pamoja na vifaa kwa ajili ya mbio hizo na kwamba shughuli zote hizo zitafanyikia katika kwenye uwanja wa michezo wa chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCU).
“Uchukuaji wa nambari za usajili pamoja na vifaa utaanza Alhamisi ya Februari 20 (saa 12 jioni hadi saa 5 jioni), Ijumaa Februari 21 (saa 10 asubuhi hadi saa 6 jioni) na Jumamosi Februari 22 (kuanzia saa 9 asubuhi hadi saa 5 jioni) katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU)”, ilisema taarifa hiyo.
Waandaaji hao wamewataka washiriki hao kuzingatia siku na muda uliowekwa ili kuepuka usumbufu na pia wametoa wito kwa wale wanaochukua nambari za ushiriki kwa niaba ya marafiki au ndugu zao kuhakikisha wanakuwa na nakala za vitambulisho vyao au barua zinazodhibitisha ya kuwa wanawawakilisha jamaa zao hao katika kuchukau nambari na vifaa.
“Ni matumaini yetu sisi wandaaji ya kuwa washiriki watajitokeza kwa wingi katika uwanja wa MoCU kutokana na kuwa baada ya tarehe zilizowekwa nambari za ushiriki au vifaa havitatolewa siku ya mbio hizo”, ilisema taarifa hiyo.
Wakati huo huo zoezi la ukusanyaji wa nambari za ushiriki linatarajiwa kuanza Jijini Dar es Salaam Februari 14, mwaka huu, eneo la Mlimani City Mall (Mbele ya Samaki Samaki) kuanzia saa 10 alasiri hadi saa 1 usiku; , Februari 15 kuanzia saa 4 asubuhi asubuhi hadi saa 12 jioni na Jumapili, Februari 16, kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni.
Baada ya Dar es Salaam, zoezi hilo litahamia Arusha Jumanne, Februari 18 na Jumatano, Februari 19, kuanzia saa 8 mchana hadi saa 1 usiku, katika hoteli ya Kibo Palace.
Waandaaji hao, katika hatua nyingine, wameonya dhidi ya wale wanaotaka kutumia nambari zisizo rasmi ikiwemo zile zilizotumika miaka ya nyuma kwenye mbio hizo au kutumia za watu wengine, ambapo wamesema watakaobainika kufanya hivyo wataondolewa kwenye mbio hizo, kukamatwa na hatimae kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Pia tunawaonya wale wanaouza nambari za ushiriki kupitia mitandaoni kinyume cha sheria.hawa nao wakibainika watachuliwa hatua za kisheria,” walisema waandaji hao.
Wadhamini wa mwaka huu ni pamoja na Kilimanjaro Premium Lager (mdhamini mkuu kilomita 42) na YAS wadhamini wa kilomita 21maarufu kama Yas Half Marathon, wadhamini wa kilomita 5 CRDB Bank pamoja na wadhamini wengine ambao ni Kilimanjaro Water, TotalEnergies, Simba Cement na TPC Sugar. Washirika rasmi, Garda World, CMC Automobiles, Salinero-Kilimanjaro na wauzaji – Kibo Palace Hotel na Keys Hotel.
Kili Marathon huandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.