Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, marehemu Mzee Aboud Jumbe anatarajiwa kuzikwa leo Jumatatu nyumbani kwake Mjini Magharibi, visiwani Zanzibar baada ya sala ya Adhuhuri.
Aboud Jumbe ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96 huku akiacha wajukuu 40, na watoto 13.
Mtoto wa marehemu Mustapha Abdu Jumbe, amesema baba yake atazikwa nyumbani kwake Migombani baada ya sala na kwamba hayo ni maneno yake aliyoyasema kulingana na usia wake. Amesema sababu ya kifo cha baba yake ni uzee na hakuna kingine.
Alisema Mzee Abdu Jumbe alizaliwa tarehe 14 mwezi Julai, 1920 Zanzibar Mkamasini.
Tayari rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar, Dkt Ally Mohamed Shein na kusema kuwa taifa limempoteza mtu muhimu na kutoa pole kwa ndugu wa marehemu, wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa kufikwa na msiba huo .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein ametangaza siku saba za maombolezo ya msiba huo visiwani humo.