×

Waziri Kabudi Awaomba Wabunge Kuhamasisha Matumizi Ya Kamusi Ya Kiswahili Shuleni

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Paramagamba Kabudi, amewaomba wabunge kuhamasisha shule za msingi kujipatia nakala za kamusi ya Kiswahili iliyotolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA). Kamusi hiyo, ambayo Waziri Kabudi amesema ni ya kipekee, inaonyesha matumizi ya maneno kwa njia rahisi na kwa kila neno imetoa namna ya kulitumia katika sentensi.

Kauli hiyo ameitoa Februari 11, 2025 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akichangia mjadala wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu shughuli za kamati kwa mwaka 2024 ambapo Waziri Kabudi amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa kamusi za Kiswahili zinatumika kikamilifu na watoto wa Kitanzania.

“Nchi jirani ndio wananunua kamusi nyingi kutoka Tanzania kuliko sisi wenyewe. Kwa mwaka mmoja, wao hununua takriban nakala 50,000 hadi 100,000, wakati sisi tukiuza nakala 100 tu tunashukuru Mungu, lakini tunahitaji kuhamasisha zaidi kununua na kutumia kamusi hizi kwa faida ya watoto wetu,” amesema Waziri Kabudi.

Pamoja na hayo Waziri Kabudi ameipongeza BAKITA kwa kazi nzuri katika kuandaa kamusi hiyo aidha ameeleza kuwa kuna mchakato unaoendelea wa kuimarisha BAKITA ili iweze kukidhi majukumu yake ya kueneza Kiswahili kimataifa.