
Mazoezi ya majini ya Cutlass Express, yaliyohusisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Marekani (U.S.ARMY) yamefungwa leo Februari 21, 2025, ikiwa ni mazoezi ya ushirikiano wa kawaida baina ya nchi rafiki.
Mazoezi hayo ya baharini yenye lengo la kupambana na uharamia, usafirishaji wa dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu na usafirishaji haramu wa silaha, yalifanyika katika Bahari ya Hindi, Tanga, Tanzania.

Akizungumza wakati wa kufunga zoezi hilo, Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo JWTZ, Meja Jenerali Ibrahim Michael Mhona amesema wanayo furaha kwa sababu mazoezi hayo yaliyoandaliwa na JWTZ na Jeshi la Marekani yameshirikisha jumla ya nchi 15.
Meja Jenerali Mhona ameendelea kusema anashukuru kwa JWTZ kuwa wenyeji wa mazoezi hayo kwa sababu askari wake wengi wamepata nafasi ya kunufaika na mazoezi hayo.

“Namshukuru Mkuu wa Majeshi, Generali Jacob John Mkunda kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mazoezi haya kwa sababu nchi yetu imepata fursa ya kubadilishana ujuzi wa kupambana na changamoto ambazo dunia nzima inapambana nazo.
Miongoni mwa changamoto hizo ni uharamia, usafirishaji haramu wa silaha, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na mambo mengine ya kiusalama.
“Hivyo mazoezi haya yamefanya tuzungumze lugha moja kwa ajili ya kutatua changamoto hizo kwa pamoja.

“Mazoezi haya yamefanyika katika Bahari ya Hindi mkoani, Tanga na ambapo kulikuwa na majeshi kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Marekani, Uingereza, Kenya, Madagascar, Ushelisheli, Djibout, Comoro, Georgia, Msumbiji, Malawi, Mauritius, Tunisia, Somalia na Senegal.” Amesema Meja Jenerali Mhona.
Zoezi hili lilizinduliwa rasmi Februari 10 mwaka huu hapa nchini na kufungwa rasmi leo, Februari 21.
Kufanyika kwa mazoezi hayo kumetoa fursa kwa vikundi shiriki kuongeza weledi na uelewa wa pamoja wa kupambana na matishio mbalimbali ya kiusalama kama vile ya ugaidi. HABARI: NEEMA ADRIAN /GPL