
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amesema mpango wa ToneTone uliozinduliwa na chama hicho jana usiku kwa ajili ya wanachama kukichangia chama chao, utakuwa na uwazi wa kutosha.
Amesema wanachama wote wa Chadema wataona kiasi kinachochangiwa na kuwaomba wasiwape fedha viongozi mkononi au kwa njia ya simu bali waingize kwenye akaunti ya chama.
Heche ameyasema hayo jana akiwa kwenye Kipindi cha Front Page kinachorushwa na Global Radio na Global TV kinachorushwa kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa saa 2.30 hadi saa 4.00.

Heche amesema wameanzisha mpango huo ili chama kiweze kupata fedha tofauti na wapinzani wao ambao ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wana rasilimali nyingi ambazo zingine zilipaswa kuwa za umma.
“CCM baada ya kugundua kuwa kuna vyama vingi wakachukua rasilimali nyingi za nchi ambazo zilipaswa kuwa mali za serikali kama vile viwanja vya mpira, baadhi ya majengo na viwanja, jambo ambalo ni kosa kubwa,” alisema Heche.
Akizungumzia Tume Huru ya Uchaguzi, Heche alisema inapaswa kuundwa kama sheria zinavyosema. Akifafanua zaidi alisema wajumbe wa tume hiyo hawapaswi kuwa chaguo la rais lakini kwa mfano mwenyekiti anatakiwa apatikane kwa kupitishwa katika kamati maalum na rais anapelekewa majina matatu yaliyochakatwa.
“Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi, Makamishna wa tume, Wakurugenzi wa wilaya nao wanateuliwa na rais halafu ndio wasimamizi wa rais ambaye nayeni mgombea. Sio haki hata kidogo. Mfumo wa upatikanaji wa tume nzima ni ya CCM.”, alisema Heche.
Stori Na Elvan Stambuli GPL.