×

Rais Dkt. Samia Akishiriki Maadhimisho Ya Siku Ya Wanawake Duniani (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanalea kizazi chenye maadili mema, heshima, na uwezo wa kujenga hoja, ili kuimarisha jamii yenye mshikamano na taifa lenye maendeleo.

Akizungumza mkoani Arusha, Machi 8, 2025 katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuwa na vijana wanaojiamini badala ya kuwa na kizazi kinachotumia jazba na sauti kubwa bila hoja madhubuti.

Rais Samia pia amewataka vijana kujielewa na kujitambua, akisema kwamba hilo ndilo msingi wa kujenga taifa lenye ustawi, haki na usawa. Ameongeza kuwa Tanzania inapaswa kuendelea kupinga ubaguzi wa aina yoyote katika jamii, huku ikijenga misingi ya maendeleo shirikishi kwa watu wote.

Maandamano ya Wanawake kutoka Taasisi mbalimbali za umma na binafsi yakipita mbele ya Jukwaa kuu kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi

Katika hatua nyingine, Rais Samia amehimiza ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia unapaswa kuanza kwa wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kuimarisha demokrasia na maendeleo ya taifa.

Rais Samia amehitimisha kwa kusema kuwa amani, mshikamano na haki za kijamii ndizo nguzo za maendeleo endelevu, hivyo kila mwananchi ana jukumu la kuhakikisha usawa wa kijinsia unadumishwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.