×

Tundu Lissu, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Wazuiwa kuingia Angola

Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu

Msafara wa Viongozi wa ACT Wazalendo ukiongozwa na Kiongozi wa Chama Dorothy Semu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Othman Masoud Othman pamoja na msafara wa Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, umezuiwa kuingia nchini Angola na Mamlaka za Serikali ya Angola.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa ACT, Mwanaisha Mndeme Machi 13, 2025 imesema Viongozi hao wanashikiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Luanda na hati zao za kusafiria zinashikiliwa, Serikali ya Angola, bila kueleza sababu yoyote imetoa amri ya Viongozi hao kurejeshwa Tanzania.

Viongozi hao waliwasili Angola kushiriki mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika The Platform for African Democrats (PAD) yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation yaliyopangwa kufanyika kuanzia March 13-16, 2025 ambapo mbali na Viongozi hao, Viongozi wengine zaidi ya 40 kutoka nchi mbalimbali Afrika ambao pia walikuwa wanahudhuria mkutano huo wamezuiliwa na Serikali ya Angola.

Moja ya Viongozi Waandamizi waliotarajiwa kushiriki kwenye Mkutano huo ni pamoja na Marais Wastaafu Ian Khama (Botswana) na Andres Pastrana Arango (Columbia), wengine ni Waziri wa Kilimo wa Afrika ya Kusini na Kiongozi wa Chama cha DA, John Steenhuisen na Kiongozi wa Chama cha PODEMOS cha nchini Msumbiji, Venancio Mondlane.

ACT Wazalendo imelaani kwa nguvu kitendo cha udhalilishaji kilichofanyika dhidi ya Viongozi wa ACT na Vionvozi wengine kwa kuzuiliwa na kushikiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Luanda ambapo ACT pia imemtaka Balozi wa Angola nchini Tanzania kutoa maelezo ni kwa sababu ganinViongozi hao wamezuiliwa na kunyang’anywa hati zao za kusafiriria.

“Tunaitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imuite na kumhoji Balozi wa Angola nchini juu ya kadhia hii na tunatoa wito kwa Serikali ya Angola kuziachia mara moja hati za kusafiria za Viongozi wetu walizozishikilia na kuwaruhusu kuendelea na ratiba yao nchini Angola”