
Kijana wa miaka 22, Kassim Ayoub Salim aliyewakilisha Tanzania Bara Katika Mashindano Makubwa ya Qurani ya Mabara yote ameitoa Tanzania kimasomaso kwa kuingia kwenye tano bora katika mchuano ulioshirikisha vijana 17 waliohifadhi kichwani Qur’an yote, juzuu 30 na sura 114 kutoka nchi na mabara mbalimbali duniani. Kwa kuwa mshindi wa tano, Kassim ameondoka na shilingi 5,380,000.
Mbali na Kassim, Tanzania iliingiza washiriki watatu, wawili miongoni mwao, Ismail Bai Makame aliyewakilisha Zanzibar na Mundhir Iliyasa Ramadhani aliyewakilisha Taasisi ya Al-Hikma Foundation ambao ndio waandaaji wa mashindano haya, hawakufanikiwa kuingia kwenye tano bora.
Aliyeibuka mshindi katika mashindano hayo ni Aiemiddin Farkhudinov kutoka Urusi; nafasi ya pili imeshikwa Abdulmuhaimin Mohamed Jumah kutoka Libya, mshindi wa tatu akawa Eslam Mahmoud Ahmed kutoka Misri na mshindi wa nne ni kijana kutoka Guyana, Saalihi Mohamed Rahim.
Washiriki wengine wametokea nchi mbalimbali duniani zikiwemo Uganda, Kenya, Ivory Coast, Nigeria, Burundi, Rwanda, Namibia, Morocco, Australia, Uingereza na Marekani.