
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza mfumo wa kitaifa wa miundombinu ya taarifa za kijiografia, ambao kukamilika kwake kutaifanya nchi kuwa na ramani mpya ya Tanzania inayolingana na mabadiliko ya kidunia.
Akihutubia kwenye hafla ya uzinduzi wa Sera ya Ardhi ya mwaka 1995, toleo la mwaka 2023, jijini Dodoma katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Rais Samia amesema kuichora ramani mpya ya Tanzania kutawezesha kupanga mipango ya nchi kidijiti na kuondoa migongano ya kisekta katika matumizi ya rasilimali mbalimbali.

“Tunapoenda kujenga barabara, sekta ya mawasiliano itakuwa hapo, itasema sisi tutapitisha mkongo hapo, wengine watasema tunapitisha nyaya za umeme, wengine bomba la maji. Sasa hivi unakuta barabara inajengwa hapa, wengine wanachimba pembeni kitu gani sijui, mwishowe barabara hazidumu. Lakini pia tutakuwa na sura nyingine ya nchi, sasa hivi nyaya kila mahali yamepita juu, lakini huenda huko mbeleni nyaya zikapita chini ya ardhi.” Amesema Rais Samia.

Akizungumzia utekelezaji wa mipango mingine ya sekta ya ardhi, Rais Samia amesema Serikali yake, kwa kutambua changamoto za sekta hiyo, imeongeza bajeti ya Wizara ya Ardhi kutoka shilingi bilioni 133.6 mwaka 2020/21 hadi kufikia shilingi bilioni 171.4 mwaka 2024/25.
Hatua hii imewezesha kuimarika kwa usalama wa milki za ardhi, upimaji wa viwanja, mashamba makubwa, pamoja na kupima mipaka ya vijiji. Pia, imefanikisha kufanyika kwa sensa ya majengo kwa mara ya kwanza tangu Tanzania ipate uhuru zaidi ya miaka 60 iliyopita.



