×

CCM Yahoji Mamlaka ya ACT-Wazalendo Kuingilia Majukumu ya ZEC

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis

Wakati uandikishaji wa wapiga kura ukimalizika salama Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehoji ni wapi ACT-Wazalendo kinakopata mamlaka ya kuingilia na kufanya kazi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kutangaza takwimu za uandikishaji.

CCM kimelaani tangazo batili lililotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Omar Ali Shehe, na kusema lina lengo la kuijengea jamii hofu na wasiwasi.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, alisema hatua ya kiongozi huyo kujibebesha kazi za ZEC ni mwanzo wa utata na ukorofi.

Mbeto alisema kitendo chake cha kutoa taarifa na takwimu za uandikishaji, wakati yeye si mtendaji wala afisa dhamana wa ZEC, huku tume haijatamka lolote, ni wazi ACT kinatafuta hekaheka.

Alisema wananchi wa Zanzibar hawataki kuingizwa kwenye msitu wa hekaheka, vurugu na mivutano isiyo na ulazima kwa kisingizio cha uandikishaji kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

“Omar Ali Shehe amekuwa akiutumia vibaya uhuru wa kisiasa na demokrasia iliyopo Zanzibar. Anaandaa mazingira tele yenye kiza kinene. ZEC ina wajibu wa kuchukua hatua za haraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018 kifungu 128(b),” alisema Mbeto.

Aidha, alisema kifungu hicho kinakataza mtu kuingilia majukumu, mamlaka, na uhuru wa tume kwa kutoa taarifa au kuagiza kutolewa taarifa juu ya jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya tume.

“Omar Shehe amepata wapi nguvu hizo? Amepewa na nani kazi au mamlaka ya kuingilia kazi za ZEC? Kwa makusudi anajaribu kutaka kuiburuza ZEC. Atimize majukumu yake ya kisiasa akiwa ACT, ZEC ni chombo kinachojitegemea,” alisema Mbeto.

Kadhalika, kifungu hicho kinataja kwamba mtu atakayefanya kosa hilo, akipatikana na hatia, atalipa faini isiyopungua shilingi laki mbili, isiyozidi shilingi milioni tano, au atatumikia kifungo kisichopungua miezi sita, kisichozidi mwaka mmoja, au adhabu zote mbili.

“Tunaitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake. Kufumba macho au kupuuza ni kuruhusu uvunjifu wa sheria nyingine zilizopo,” alieleza.