
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imewajibu Chama cha ACT Wazalendo kuhusu ombi lao la kuchukuliwa hatua Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla kutokana na matamko yake kuhusu ebola na mpox.
Katika barua yake, Msajili ameeleza kuwa tayari ofisi yake ilishachukua hatua zinazostahili kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258, hata kabla ya kupokea ombi la ACT Wazalendo. Hata hivyo hatua hizo hazijatolewa hadharani.
Kupitia barua yake ya tarehe 25 Machi 2025 iliyosainiwa na msaidizi wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, kupitia kwa Naibu wake Sisty Nyahoza, ameeleza kuwa ofisi yake hufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuchukua hatua zinazohitajika bila kusubiri mapendekezo kutoka kwa taasisi au mtu yeyote.
“Msajili anakushukuru kwa mapendekezo yako na anapenda ufahamu kuwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa huchukua hatua katika matukio kama hayo kwa mujibu wa sheria, hata bila ya mapendekezo ya mtu au taasisi yoyote,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, amekiambia kipindi cha Front Page kinachorushwa hewani na Globoltv online leo kuwa alikuwa amewasilisha barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa akipendekeza hatua zichukuliwe dhidi ya Amos Makalla kutokana na kauli alizotoa kwenye mkutano wa hadhara mkoani Simiyu tarehe 22 Machi 2025 za madai kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendesha harambee ya Tonetone kukusanya fedha ili ikanunua virusi vya M-pox na Ebola ili ieneze ugonjwa huo kwa Watanzania kwa lengo la kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
o Alisema ACT ilizitaja kauli hizo kuwa za kizembe na zenye lengo la kuzua taharuki nchini.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikufafanua hatua mahsusi ilizomchukulia Makalla aliyezusha taharuki hiyo ambayo sasa ni gumzo nchini.
o Lakini msajili wa vyama vya siasa amesema kuwa anatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
Stori Na Elvan Stambuli GPL