
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema lipo mbioni kuanzisha mkoa maalum wa kiutendaji ili kushughulikia changamoto za umeme katika Reli ya Kisasa (SGR).
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamohanga, amesema hayo Machi 26, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi za Idara ya Habari (MAELEZO).
Kwa mujibu wa Nyamohanga, mpango wa TANESCO ni kuifanya SGR kuwa mkoa maalum wa kiutendaji ili kuhakikisha usambazaji wa umeme unakuwa wa uhakika. Mkoa huo utakuwa na meneja uratibu maalum atakayesimamia mradi huo pamoja na timu maalum ya wataalamu.

“Tutakuwa na timu maalum ambayo kazi yake ni kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika katika mradi huu,” amesema Mhandisi Nyamohanga.
Akizungumzia changamoto za kukatika kwa umeme kwenye SGR, Mhandisi Nyamohanga amesema mradi huo una laini maalum ya umeme, lakini changamoto zilizojitokeza zilihusiana na mfumo mpya uliokuwa ukitumiwa kwa mara ya kwanza.
“Kitu kipya mara nyingi huleta changamoto. Hata hivyo, tunawahakikishia Watanzania kwamba laini hiyo ipo madhubuti na inaendelea kuimarika,” amesema.

Kuhusu changamoto ya umeme nchini kwa ujumla, Mhandisi Nyamohanga amesema sababu kubwa ni kuzidiwa kwa Gridi ya Taifa kutokana na ongezeko la watumiaji wa umeme. Hata hivyo, amesema TANESCO imejipanga kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika katika kila eneo nchini.
Aidha, amesema TANESCO ina mpango wa kuboresha mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha upatikanaji wa umeme pindi mteja anaponunua tokeni, tofauti na sasa ambapo inachukua muda mrefu.

Akizungumzia suala la Tanzania kununua umeme kutoka nje, Mhandisi Nyamohanga amesema hatua hiyo inatokana na sababu za kijiografia, hasa katika maeneo ya pembezoni ambako miundombinu ya umeme bado haijafika kwa urahisi.
“Kwa mfano, mtu anayekaa Sumbawanga anaweza kuona umeme wa Zambia unawaka, lakini yeye hana. Kama Taifa, tuliona ni bora kununua umeme huo ili wananchi wasiendelee kuteseka,” amesema.