×

wizara ya elimu yatenga milion 50 kuchagiza masomo ya sayansi na hisabati

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa motisha ya sh. milioni 50 kwa wahadhiri kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini wanafundisha masomo ya Sayansi , Hisabati na Teknolojia, kufanya utafiti na kuchapisha kwenye majarida mbalimbali ya kimataifa na watakaofanya vizuri watapata zawadi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda, wakati akifunga mafunzo ya walimu wa shule za Sekondari nchini wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati yaliyofanyika mkoani Singida.

Amesema hatua hiyo inaelenga kuzalisha tafiti nyingi za kisayansi ambazo zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali na kutoa fursa kwa wahadhiri hao kutambulika kimataifa na kujiingizia kipato.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa katika kufanisha hayo, Serikali inaendelea kufanya mageuzi ya elimu nchini kwa kuwajengea uwezo walimu wa masomo ya sayansi na hisabati kupitia mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini( SEQUIP) ili kuzalisha wanafunzi wengi wa sayansi ambao baadae watasaidia kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali.

Ameongeza kuwa Wizara pia kupitia Programu ya Samia Extended imepanga kutoa ufadhili wa masomo ya sayansi kwenye nguvu za Atomic katika vyuo Vikuu nje ya nchi.

Amesema Serikali imejiandaa kikamilifu kutekeleza program hiyo kinachofanyika kwa sasa ni wanafunzi kuhamasishwa kusoma masomo hayo na kufanya vizuri ili kupata ufadhili kwenda nje ya nchi.

“ Tumejipanga kuwafadhili vijana wetu watakofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi, hisabati na teknolojia, nafasi zipo kwa waliofanya vizuri kwenda nje ya nchi kusoma serikali itagharamia kila kitu ili wakajifunze namna ya kutekengeneza atomiki mbalimbali,” amesema Prof. Mkenda.