
Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam wamemkamata dereva wa bajaji aitwaye John Bariki Mosha (30), mkazi wa Kimara Temboni, kwa kosa la kupita katika barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kinyume cha sheria.
Tukio hilo lilitokea tarehe 4 Aprili 2025 majira ya saa 4:00 asubuhi, katika eneo la Kimara Baruti ambapo askari polisi waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya usalama barabarani walimkamata dereva huyo kwa makosa ya barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, dereva huyo alikaidi amri ya kusimama na akaendesha bajaji kwa mwendo kasi hadi alipokamatwa katika eneo la Ubungo Mawasiliano. Baada ya kukamatwa, madereva wengine wa bajaji walifika eneo hilo wakijaribu kumzuia askari polisi wasimchukue dereva huyo.
Katika hali ya taharuki, mmoja wa madereva hao alichomoa plagi ya pikipiki ili isichukuliwe na polisi, kitendo ambacho kilisababisha cheche za moto na hatimaye bajaji kuteketea kwa moto.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa onyo kali kwa madereva wote wa vyombo vya moto, likiwataka kufuata sheria za usalama barabarani na kutojihusisha na uvunjaji wa sheria, hususan kupita kwenye barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT) bila kibali.
