×

Mkuu wa Wilaya Awataka Wakazi wa Arusha Kuchangamkia Fursa za Huduma Jumuishi za Kifedha

Kaimu Mkurugenzi wa Yas – Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya (wa pili kushoto), akimkabidhi zawadi Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude (wa pili kulia), wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa chapa za Yas na Mixx mkoani Arusha. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano – Mixx by Yas, Justine Lawena, na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa – Yas Business, Anatory Lelo.

Arusha, Tanzania 17 Aprili 2025: Mkuuwa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude, amezindua rasmi chapa mpya za Yas na Mixx by Yas katika hafla iliyofanyika mkoani humo, huku akisisitiza umuhimu wa teknolojia katika kurahisisha huduma za mawasiliano na fedha kwa njia ya kidijitali.

Uzinduzi huo umezikutanisha taasisi za umma, sekta binafsi pamoja na mawakala wakubwa wa mawasiliano ili kupata uelewa wa mwelekeo mpya na maboresho yaliyoletwa na chapa hizi mpya, kufuatia mageuzi kutoka chapa ya awali ya Tigo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe.Mkude alisema kuwa teknolojia imeendelea kuwa injini ya maendeleo kwa Watanzania, ikitoa fursa mpya za kiuchumi, kijamii na kielimu kwa miongo kadhaa.

“Kupitia uzinduzi wa chapa hizi mbili – Yas na Mixx by Yas – tunashuhudia si tu mageuzi ya kimuonekano, bali pia ya kimtazamo, mbinu na dira ya utoaji huduma bora zinazogusa maisha ya kila Mtanzania kwa namna ya kipekee,”alisema Mkude.

Aidha, alieleza kuwa ujio wa chapa hizi unatoa suluhisho halisi kwa changamoto za mawasiliano na huduma za kifedha, jambo linaloendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora bila kujali mahali alipo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Yas – Kanda yaKaskazini, Bw. Daniel Mainoya, alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 30, chapa ya Tigo (ambayo sasa ni Yas) imekuwa mstari wa mbele katika mageuzi ya kidijitali kwa kuwaunganisha Watanzania na kuwapatia fursa za kifedha kupitia teknolojia.

“Tunasonga mbele sasa na chapa mpya ya Yas. Yas si chapa tu bali ni falsafa ya mabadiliko, uvumbuzi na mshikamano wa kiuchumi,”alisema Mainoya.

Aliongeza kuwa Yas inalenga kuwainua vijana, wafanyabiashara wadogo na wakati, pamoja na kila Mtanzania anayesaka fursa ya kujikwamua kupitia teknolojia na huduma za kifedha za kisasa.

Uzinduzi huu ni hatua kubwa kwa sekta ya mawasiliano nchini, ukiashiria mwanzo wa sura mpya ya huduma zinazolenga kumgusa kila mwananchi kwa karibu zaidi.