×

TAMWA: Yapinga Ukatili wa Kijinsia Kuelekea Uchaguzi Mkuu

ROSE Reuben, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) ameweka wazi kuwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 inawezekana kufanya siasa bila mashambulizi ya kijinsia dhidi ya Wanawake.

Juni 27 2025, makao makuu ya TAMWA, Dar umefanyika mkutano huo ambapo limetolewa tamko kwa vyombo vya habari kulaani vikali mashambulizi ya kijinsia dhidi ya wanawake, hususani viongozi wa kisiasa, kupitia mitandao ya kijamii.

Chama hicho kimesisitiza kuwa vitendo hivyo ni kikwazo kwa ushiriki wa wanawake katika uongozi na kimetoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.

Rose amesema: “Kwa mwaka huu ikiwa ni mwaka wa uchaguzi kitu ambacho tumekuwa tukifuatilia ni namna ambavyo mijadala inakwenda bila kutweza utu wa Mwanamke. Wakati tukiwa tunafurahia teknolojia ni jambo jema kwa kuwa wengi wanajifunza huko ila tunaona kuna ukatili wa kijinsia.

“Ukatili wa kijinsia umekuwa ukiwakumba wanawake maarufu na wanasiasa. Kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais hapa Tanzania tunawaomba Watanzania, Wanasiasa waungane waache matamshi ya chuki kwa kuamini ni njia ya kuitumia ili washinde.

“Kiongozi ambaye anakuja na hoja, kiongozi ambaye anajua Watanzania nini wanahitaji huyu anahitajika. Kiongozi anayetumia maneno ya chuki kuanzia ngazi ya kijamii mpaka kiti cha Urasi sisi tunaona huyo sio mwanasiasa. Mila na desturi zetu haziendani na maneno ya chuki.

“Tunawaomba Wanasiasa, viongozi wetu tunaviomba vyama vya siasa kujikita kwenye siasa za hoja. Matamshi ya chuki yamekuwa yakiwasababishia wengine kuamini kuwa wakiwa viongozi watakuwa wanadhalilishwa mchana na jioni. Tamwa tumeona tuzungumzie kuwa siasa bila matusi inawezekana,” alisema Rose.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu itazinduliwa rasmi Julai 24 2025 usipange kukosa.