×

Gari Lililobeba Maiti Lapinduka Na Kuua Watu Wawili Na Kujeruhi Wengine Morogoro, Kamanda Aeleza – Video

JESHI la Polisi mkoani Morogoro limemkamata Mohammed Said Kisukari (43), dereva, mkazi wa Kimara, Mkoani Dar es salaam kwa kosa la kuendesha gari kwa njia ya hatari kupinduka na kusababisha vifo vya watu wawili.

Taarifa ya leo Julai 10, 2025 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Julai 9, 2025 katika kijiji cha Bagilo, kata ya Tegetero, Wilaya ya Morogoro vijijini.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa gari lilokuwa likisafirisha maiti lenye namba za usajili T.492 EHP aina ya Toyota Rosa(min bus) likiendeshwa na Kisukari liliacha njia na kutumbukia kwenye korongo na kusababisha kifo kwa watu wawili jinsia ya kiume ambao walikuwa wakisindikiza maiti.

Aidha, katika ajali hiyo waombolezaji wengine walipata majeraha kiasi ambapo wanaendelea na matibabu. Majeruhi watano wamepelekwa hospital ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.

Uchunguzi wa awali katika eneo la ajali umebaini kuwa dereva wa gari hilo aliendesha kwa mwendo kasi bila kuzingatia jiografia ya eneo hilo ambayo ni milima, miteremko na kona kali.