
Mwekezaji maarufu na Rais wa heshima wa klabu ya Simba SC, Mohammed Dewji (Mo), amevunja ukimya kwa kutoa ufafanuzi mzito kuhusu mchango wake ndani ya klabu hiyo tangu alipoanza kuwekeza rasmi mwaka 2017.
Kupitia kauli yake ya wazi, Mo Dewji amesema kuwa kati ya mwaka 2018 hadi sasa, tayari amewekeza jumla ya shilingi Bilioni 87, fedha zilizotumika katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya klabu, ikiwemo uendeshaji, usajili, mishahara ya wachezaji, na misaada ya dharura.
“Kuanzia mwaka 2018 hadi leo, nimewekeza shilingi Bilioni 45 kwa ajili ya mishahara, usajili, maandalizi ya timu na mahitaji mengine ya uendeshaji,” alisema Mo.
Aidha, alifafanua kuwa mbali na gharama hizo za kawaida, alitoa mchango wa shilingi Bilioni 20 kama sehemu ya ununuzi wa hisa asilimia 49 ndani ya klabu ya Simba, hatua iliyolenga kuiwezesha klabu kufanya mageuzi ya kiutawala na kiuchumi kupitia mfumo wa mabadiliko ya kimuundo (Simba SC Transformation).
Mbali na uwekezaji rasmi, Mo amesema kuwa ameendelea kusaidia klabu katika hali mbalimbali za dharura kwa kutoa takribani Bilioni 22 nje ya mfumo rasmi, hasa kila mara kulipojitokeza changamoto za ghafla zinazoihitaji Simba SC.
“Mara nyingi nimekuwa nikitoa msaada nje ya mfumo rasmi kila palipojitokeza uhitaji wa dharura, kuanzia mwaka 2017 hadi 2024 nimetumia takribani Bilioni 22 kwa misaada hiyo.”
Kwa ujumla, Mo amesema mchango wake kwa Simba SC hadi sasa umefikia shilingi Bilioni 87, akisisitiza kuwa tuhuma zinazoenea kwamba “Mo hatoi hela” ni za kupotosha, zenye mwelekeo wa chuki na hazina msingi wowote.
“Hivyo kusema Mo hatoe hela ni kauli ya kupotosha yenye mwelekeo wa chuki. Tuachane na fitna zisizo na msingi, tujenge palipotoboka, tuzibe ufa panapovuja na tusonge mbele bila kuonyeshana vidole,” amehitimisha Dewji kwa msisitizo.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo mjadala kuhusu hali ya kifedha ya klabu na nafasi ya wawekezaji unazidi kushika kasi mitandaoni na miongoni mwa wanachama, hasa kipindi hiki cha maandalizi kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania.