×

Mahakama Kuu Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Amri Ya Zuio La Shughuli Za Kisiasa Kwa Viongozi Wa Chadema

Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa ufafanuzi rasmi kuhusu amri ya zuio la kufanya shughuli za kisiasa kwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, pamoja na Makamu Wenyeviti wawili, John Heche (Tanzania Bara) na Saidi Mzee (Zanzibar).

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamisi Julai 17, 2025, jijini Dar es Salaam, Wakili Gido Simfukwe – mmoja wa mawakili wanaowakilisha wadai katika shauri hilo – amesema hatua ya kuomba ufafanuzi ilichukuliwa baada ya kubainika kuwepo kwa taarifa wanazodai kuwa ni za kupotosha kutoka kwa upande wa wadaiwa, ambao ni Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa CHADEMA.

Kwa mujibu wa Wakili Gido, yeye pamoja na Wakili mwenzake Shabaan Marijani waliiandikia Mahakama barua ya kuomba ufafanuzi juu ya wale wanaohusika moja kwa moja na zuio hilo, kama lilivyotolewa na Mahakama Kuu tarehe 10 Juni 2025 katika shauri dogo Na. 8960/2025.

Katika kujibu barua hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, kupitia waraka wa tarehe 14 Julai 2025, alifafanua kuwa zuio hilo linawahusu:

Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA,

Mwenyekiti au Kaimu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa,

Makamu Mwenyekiti au Kaimu Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara,

Makamu Mwenyekiti au Kaimu Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

Kwa mantiki hiyo, Tundu Lissu, John Heche, na Saidi Mzee – waliotajwa kama viongozi walioko madarakani kwa sasa – wanaangukia katika kundi la waliopigwa marufuku kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa amri hiyo ya Mahakama Kuu.