
Kampuni ya MultiChoice imetoa onyo kali kwa yeyote atakayehusika kurusha au kuonesha maudhui yenye haki miliki bila idhini na Imetangaza kuwa itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika watakaokiuka haki hizo.
Kupitia taarifa yake, MultiChoice imesisitiza kuwa ina haki za kipekee kupitia kampuni tanzu ya SuperSport kuonesha michuano mikubwa ya soka kama Premier League, UEFA Champions League, na ligi nyingine maarufu pia haki hizi zinahusisha matangazo kwa televisheni za kulipia pekee.
Aidha SuperSport inamiliki haki ya kurusha matangazo hayo katika eneo lote la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania Kwa hivyo ni marufuku kwa chombo chochote kingine kusambaza au kurusha mechi hizo bila ruhusa maalum kutoka MultiChoice.
Taarifa hiyo imeelekezwa kwa makampuni ya kurusha matangazo kwa waya, vituo vya runinga na umma kwa ujumla vilevile MultiChoice imeeleza kuwa kushindwa kufuata sheria ya haki miliki Na. 7 ya mwaka 1999 kutasababisha hatua kali za kisheria.
Hii imekuja siku chache kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi za Ulaya, ikiwemo Premier League inayotarajiwa kuanza Agosti 15 ambapo SuperSport itarusha mechi zote muhimu kupitia chaneli zake maalum na baadhi ya mechi zitakuwa na maelezo kwa Kiswahili ili kuwapa Watanzania ladha ya nyumbani.
