×

Absa Bank Tanzania Yasisitiza Dhamira Yake Kuendeleza Ukuaji Wa Uchumi Halisi Nchini Tanzania

Benki ya  Absa Tanzania imeahidi kuendeleza dhamira yake katika kusaidia ukuaji wa uchumi halisi nchini Tanzania, wakati ikizungumzia udhamini wake katika jukwaa mahsusi lililowakutanisha watendaji wakuu wa makampuni nchini, linalokwenda kwa jina la ‘The 200 CEOs Business Forum’ lililofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Obedi  Laiser, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania alisema Jukwaa hili si mkutano wa mawazo pekee bali ni chombo cha maamuzi yanayosukuma mitaji, kuunda ajira, kurasimisha minyororo ya thamani na kufungua fursa za mauzo ya nje akisema kama Absa, wanajivunia kusimama pamoja na viongozi wa biashara wa Tanzania katika wakati huu nyeti hususani kupitia dhamira yao ya “Kuiwezesha Afrika ya Kesho, Pamoja, hatua moja baada ya nyingine”.
“Stori yako ina thamani” si ahadi tu, ndivyo tunavyojitokeza, tumesikiliza kwa makini vipaumbele na mahitaji ya wakurugenzi wakuu, na kwa kujibu tunawasilisha suluhisho zinazochochea kasi ya biashara, zikiwemo Absa Infinite Card, Absa Business Credit Card, Vehicle Asset Finance (VAF), uwezo mpana wa Cash Management & Payments, Trade & Working Capital, Treasury & Risk Management, pamoja na majukwaa yetu ya kidijitali ya benki kwa makampuni yanayosaidia idara za fedha kufanya kazi kwa kasi na udhibiti.
“Tunawezesha malengo ya Watendaji wakuu (CEOs) na wajasiriamali kupitia suluhisho bora za kifedha, zenye bei shindani na zinazotolewa kwa wakati na umahiri.” Bw. Laiser aliongeza akisema udhamini huu mkubwa wa Absa unaonesha ushirikiano wa muda mrefu wa benki na Serikali na sekta binafsi wa kuharakisha ukuaji jumuishi.
Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt Suleiman Hassan Serera alisitiza umuhimu wa hatua za pamoja katika kupanua ajira na mauzo ya nje huku mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), akitoa mrejesho wa mwelekeo wa uchumi unaosaidia kupanga maamuzi katika bodi.
Jukwaa hilo la tatu liliwakutanisha watendaji wakuu kutoka katika makampuni mbalimbali  na viongozi waandamizi kutoka taasisi za kiserikaliambapo moja ya mada zilizojadiliwa ilikuwa ni jinsi fedha inavyoweza kutumika kama chachu ya ukuaji wa biashara nchini  ikiwa ni pamoja na mikakati na fursa mbalimbali zinazoweza kupatikana kutoka taasisi za kifedha.

Leave a Comment