
Msomaji maarufu wa dua na mihadhara ya kiislamu, Sheikh Alhadi Musa, ametoa ujumbe wa kutafakari na maonyo kwa waumini wakati wa mazishi ya Hussein Msopa, anayejulikana zaidi kwa jina la Sheikh Sharif Majini, aliyefariki dunia wiki hii na kuzikwa leo katika Makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya mamia ya waombolezaji waliohudhuria mazishi hayo, Sheikh Alhadi Musa aliwataka Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuishi kwa wema, kujiepusha na dharau, na kujiandaa na maisha ya akhera, akisisitiza kwamba kifo cha Sheikh Sharif Majini kimeacha funzo kubwa.

“Leo tunamzika ndugu yetu, lakini tusisahau kuwa na sisi tunafuata. Dunia ni njia tu, na mwisho wake ni hapa kaburini,” alisema Sheikh Alhadi Musa kwa sauti yenye majonzi.
Sheikh huyo pia aliwaomba waumini kuacha chuki, kashfa na mijadala ya matusi mitandaoni, akisema marehemu alikuwa mtu wa kusaidia watu wengi kwa dua na matendo mema, hivyo anapaswa kukumbukwa kwa mema yake.

Mazishi ya Sheikh Sharif Majini yalihudhuriwa na viongozi wa dini, ndugu, marafiki, pamoja na waumini kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa jirani.
Marehemu Hussein Msopa (Sheikh Sharif Majini) alikuwa maarufu kwa kutoa tiba za kiroho, mihadhara na dua, na amekuwa akifuatiliwa sana kwenye mitandao ya kijamii kutokana na mafundisho yake kuhusu imani na maisha ya kiroho.