×

Pyramids Yatawala Afrika, Hakimi na Mzize Washinda Tuzo Kuu za CAF

Beki wa kulia wa Paris Saint-Germain na timu ya Taifa ya Morocco, Achraf Hakimi.

Beki wa kulia wa Paris Saint-Germain na timu ya Taifa ya Morocco, Achraf Hakimi, ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika (CAF Player of the Year 2025) baada ya kuwashinda nyota wawili wakubwa—Mohamed Salah (Misri, Liverpool) na Victor Osimhen (Nigeria, Galatasaray).

Hakimi ametwaa tuzo hiyo kutokana na msimu wake wa kiwango cha juu akiwa na PSG, ambapo ameiongoza klabu hiyo kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu Ufaransa, na UEFA Super Cup, sambamba na kuifikisha PSG fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu 2025.

Mshambuliaji wa Young Africans SC, Clement Mzize.

Katika upande wa Tanzania, mshambuliaji wa Young Africans SC, Clement Mzize, ameandika historia kwa kutwaa Tuzo ya Bao Bora la Mwaka – CAF Goal of the Season 2025. Mzize ameshinda tuzo hiyo kupitia bao lake la shuti kali la mbali alilofunga dhidi ya TP Mazembe kwenye hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita—bao ambalo lilivutia mashabiki barani kote.

Kwa upande wa vilabu, mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/25, Pyramids FC, wametajwa kuwa Timu Bora ya Mwaka Afrika (CAF Men’s Club of the Year 2025). Pyramids wamekuwa na msimu wa mafanikio makubwa baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika, CAF Champions League, pamoja na CAF Super Cup.

Tuzo hizo zimeendelea kuonyesha ubora wa wachezaji na timu mbalimbali barani Afrika, huku msimu wa 2025 ukionyesha mwamko mkubwa wa vipaji kutoka mataifa tofauti.

Leave a Comment